Nov 03, 2017 14:17 UTC
  • Zarif: Marekani inajaribu kupotosha ukweli kuhusu mashambulizi ya Septemba 11

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inafanya juu chini kupotosha ukweli wa mambo kuhusu mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Mohammad Javad Zarif ametoa radiamali hiyo baada ya ripoti ya kurasa 19 ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida kudai kuwa Iran ililiunga mkono kundi hilo la kigaidi kabla ya mashambulizi hayo ya Septemba 11. 

Ripoti hiyo ambayo ni sehemu ya nyaraka 47 elfu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, imemnukuu aliyekuwa kiongozi wa mtandao huo Osama Bin Laden akisema kuwa: "Yeyote anayetaka kuishambulia Marekani, Iran ipo tayari kumpa usaidizi na uungaji mkono."

Hii ni katika hali ambayo, Septemba 11 mwaka huu wakati ambapo Marekani ilikuwa inaadhimisha kumbukumbu ya hujuma hizo dhidi yake, Kanali ya Televisheni ya Fox News ya Marekani ilitangaza kuwa, ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington Marekani ulidhamini mashambulio hayo ya kigaidi ya miaka 16 iliyopita.

Majengo pacha ya WTC katika mashambulizi ya Sep. 11

 

Fox News iliripoti kuwa, watu 15 kati ya 19 walioteka nyara ndege za abiria na kuzitumia katika mashambulio hayo walikuwa raia wa Saudia. 

Itakumbukwa kuwa, Septemba 11 mwaka 2001, Marekani ilikabiliwa na mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyosababisha uharibifu mkubwa, ambapo ndege tatu za abiria zilizokuwa zimetekwa nyara ziligonga majengo mawili pacha ya World Trade Centre mjini New York na jengo la Wizara ya Ulinzi, Pentagon, katika mji wa Washington. Mashambulizi hayo yaliua karibu watu elfu tatu. 

Tags