Shamkhani: Taifa la Iran limeweka rekodi ya dunia ya kuidhalilisha sana Marekani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: Marekani ina faili kubwa zaidi la kushindwa na kugonga mwamba katika kukabiliana na irada ya taifa la Iran kulinganisha na kushindwa kwake katika kukabiliana na mataifa mengine na kwamba taifa la Iran limeweka rekodi ya kujivunia katika suala hilo.
Ali Shamkhani ameyasema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waandamanaji katika maadhimisho ya Aban 13 yaliyofanyika mbele ya Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran. Ameongeza kuwa tarehe 13 Aban 1358 ( tarehe 4 Novemba 1979) haikuwa siku ya mwanzo ya uadui wa wazi na wa dhahiri shahiri wa Marekani na hatua zake za kikhabithi dhidi ya taifa la Iran, na kwamba uadui huo ungali unaendelea na Marekani haitoacha ushari na kuingilia masuala ya ndani ya Iran.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria kuwa siasa za kiadui dhidi ya Iran za Donald Trump zimewafanya wananchi wa Iran waamue leo kuingia barabarani na akafafanua kwa kusema: kuwa ngangari taifa la Iran katika kukabiliana na utawala wa Marekani kuanzia wa Democrats mpaka Republican kunafanyika kwa ajili ya kulinda utambulisho wa Kiislamu na wa Kiirani.
Shamkhani aidha ameeleza kwamba: upinzani wa Marekani kwa maendeleo ya kielimu na kisayansi ya Iran katika nyanja za anga za mbali, nyuklia na makombora, hatua inazochukua kwa madhumuni ya kuupindua Mfumo wa Kiislamu, kukabiliana na mipango yake ya kijeshi, kueneza propaganda za kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, kufanya njama za kuzusha mivutano na mitafaruku kwa kuzichochea nchi jirani na kujaribu kuchafua sura ya Mapinduzi ya Kiislamu ni orodha ndogo tu ya hatua za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Maadhimisho ya maandamano ya Siku ya Aban 13 inayojulikana kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari yalifanyika leo asubuhi wakati mmoja hapa mjini Tehran na katika miji mingine nchini kwa kuhudhuriwa kwa wingi na wananchi wa kawaida, wanafunzi, wanachuo na viongozi mbalimbali nchini. Mwishoni mwa maandamano hayo lilitolewa azimio la vipengee tisa la kulaani siasa za kiistikbari za Marekani dhidi ya taifa la Iran.../