Marekani yazuia mchango wa wahanga wa tetemeko la ardhi lililoua mamia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36439-marekani_yazuia_mchango_wa_wahanga_wa_tetemeko_la_ardhi_lililoua_mamia_iran
Wizara ya Fedha ya Marekani imezuia kufanyika mchango kwa ajili ya wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea katika mpaka wa Iran na Iraq na kusababisha maafa makubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 16, 2017 12:26 UTC
  • Marekani yazuia mchango wa wahanga wa tetemeko la ardhi lililoua mamia Iran

Wizara ya Fedha ya Marekani imezuia kufanyika mchango kwa ajili ya wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea katika mpaka wa Iran na Iraq na kusababisha maafa makubwa.

Tohid Najafi, mtaalamu wa tiba raia wa Iran ambaye anaishi na kufanya kazi katika mji wa Detroit nchini Marekani ameliambia shirika la habari la al-Jazeera la Qatar kuwa, Wizara ya Fedha ya Marekani imefunga ukurasa alioufungua kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kwa ajili ya mchango huo Jumatatu.

Hadi kufikia Jumatano ya jana, Wairani waishio nje ya nchi pamoja na wapenda haki wengine walikuwa wametoa mchango wa dola laki mbili.

Najafi amesema alipokea ujumbe kutoka shirika la Facebook ukimwambia kuwa hatoweza kupokea fedha hizo zilizochangwa, hadi apate kibali cha moja kwa moja kutoka Wizara ya Fedha ya Marekani.

Mahema yaliyowekwa kwa ajili ya wahanga wa zilzala

Hii ni katika hali ambayo, Jumanne iliyopita Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kushukuru mchango wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya wahanga wa zilzala hiyo, lakini alisisitiza kuwa Iran hivi sasa ina uwezo wa kushughulikia mgogoro huo wa tetemeko la ardhi kwa kustafidi na suhula za ndani.

Karibu watu 500 wameaga dunia na wengine zaidi ya elfu tisa kujeruhiwa katika zilzala hiyo. Aidha nyumba zaidi ya 12 elfu ziliharibiwa kikamilifu katika janga hilo la kimaumbile.

Tetemeko hilo la ardhi lililokuwa la ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha Rishta lilitokea siku ya Jumapili usiku katika maeneo mbalimbali ya magharibi mwa Iran na pia katika maeneo ya mashariki mwa Iraq.