Ujumbe wa Jenerali Suleimani kwa Kiongozi Muadhamu, satwa ya ISIS imeangamizwa
Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, amemtumia ujumbe Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akitangaza kuangamizwa satwa khabithi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sepahnews, Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumanne asubuhi amemtumia ujumbe Ayatullah Khamenei na kutangaza kuwa: "Mimi kama mtumishi na askari mwenye kutekeleza wadhifa kwa niaba yako katika medani hii, ninatangaza hapa kuwa, kufuatia kukombolewa mji wa Al Bukamal, ngome ya mwisho ya ISIS na bendera ya kundi hili la Kimarekani-Kizayuni imeshushwa na mahala pake kupeperushwa bendera ya Syria na kwa msingi huo satwa khabaithi na iliyolaaniwa ya ISIS imefika ukingoni."
Meja Jenerali Suleimani kwa niaba ya makamanda na mujahidina wote wasiotaka kutajwa majina katika medani na maelfu ya mashahidi na majeruhi walinzi wa Haram kutoka Iran, Iraq, Syria, Lebanon, Afghanistan na Pakistan, ambao walijitolea kulinda maisha, heshima na matukufu ya Waislamu, amempongeza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran na mataifa madhulumu ya Iraq na Syria na Waislamu wote duniani kufuatia ushindi huo mkubwa wenye kuainisha hatima.
Kamanda wa Kikosi cha Quds katika IRGC ameongeza kuwa, uongozi wenye busara na hekima ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na Ayatullah Sistani wa Iraq ndio sababu ya kuletwa pamoja uwezo wote huu mithili ya tufani.
Aidha amesisitiza kuwa: "Kwa yakini, kusimama kidete serikali za Iraq na Syria na msaada wa wanajeshi na vijana wa nchi hizi mbili haswa Hashdu Shaabi pamoja na vijana wengine Waislamu kutoka nchi mbali mbali ambao wamejitokeza kwa nguvu chini ya mhimili wa Hizbullah kwa uongozi wa Sayyid Hassan Nasrallah, ni nukta zilizokuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha hatari iliyokuwepo."
Meja Jenerali Suleimani ameongeza kuwa: "Jinai hizo zote, kama alivyokiri rais wa sasa wa Marekani, zimeratibiwa na viongozi pamoja na taasisi zinazohusiana na Marekani na viongozi wa sasa wa Marekani pia wameuhisika katika utekelezwaji wa njama hizo."
Kamanda wa Kikosi cha Quds aidha amewashukuru viongozi wa kiserikali na kijeshi nchini Iran kwa msaada waliotoa kwa serikali na mataifa ya Iraq na Syria.