Iran: Serikali ya Uingereza inaunga mkono mvamizi katika vita vya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40899-iran_serikali_ya_uingereza_inaunga_mkono_mvamizi_katika_vita_vya_yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema: Pamoja na kuwa serikali ya Uingereza inatoa nara za kumaliza vita Yemen lakini inatumia ushawishi wake kimataifa kuunga mkono mvamizi."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2018 10:34 UTC
  • Iran: Serikali ya Uingereza inaunga mkono mvamizi katika vita vya Yemen

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema: Pamoja na kuwa serikali ya Uingereza inatoa nara za kumaliza vita Yemen lakini inatumia ushawishi wake kimataifa kuunga mkono mvamizi."

Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao na waandishi habari mjini Tehran. Akijibu swali  la mwandishi wa Radio Tehran kuhusu matamshi ya balozi wa Iran nchini Uingereza ambaye amesema London na Tehran zina mtazamo mmoja kuhusu kumalizika vita Yemen, Qassemi ameongeza kuwa: "Katika safari ya nchini Uingereza, Sayyed Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, alifanya mazungumzo na wakuu wa nchi hiyo kuhusu masuala mbali mbali ikiwemo kadhia ya vita nchini Yemen."

Qassemi amesema kunafanyika jitihada kutumia fursa iliyojitokeza kumaliza vita nchini humo. Akiashiria rasimu ya pendekezo la Uingereza kuhusu Yemen na madai kuwa eti Iran imekiuka vikwazo vya silaha nchini Yemen, Qassemi amesema serikali ya Uingereza inahadaa.

Kuhusu uamuzi wa Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu (Jerusalem) ifikapo mwezi Mei, Qassemi amesema Marekani itapata hasara kutokana na uamuzi wake huo.

Sayyed Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje nchini Iran

Amesema hatua hiyo ni kati ya sera potovu kabisa za Marekani huku akisisitza kuhusu ulazima wa nchi za Kiislamu kuchukua hatua kali kukabiliana na wendawazimu wa Marekani.

Kwingineko Qassemi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuona usitishwaji vita unatekelezwa kote Syria ili misaada iwafikie raia. Aidha amegusia oparesheni za kijeshi za Uturuki katika eneo la Afrin kaskazini mwa Syria na kusema marais na mwaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uturuki na Russia watakutana mwezi Mei kujadili hali katika nchi hiyo ya Kiarabu. Amesema mazungumzo hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kutatua hitilafu zilizopo na pia kutoa mchango katika kukabiliana na ugaidi na kurejesha utulivu Syria.