Iran ina ushahidi kuhusu uhusiano wa Marekani na Daesh (ISIS)
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema vyombo vya usalama vya Iran vina ithibati kuhusu uhusiano kati ya Marekani na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Hossein Amir-Abdollahian, ambaye huko nyuma alihudumu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema walipokea nyaraka za siri kutoka kwa Meja Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds kilicho chini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, zinazothibitisha mahusiano ya karibu ya Washington na genge hilo la wakufurishaji.
Amesema nyaraka hizo walizokabidhiwa na Meja Jenerali Soleimani zina taarifa kuhusu eneo la kijiografia, wakati na maelezo ya kina kuhusu namna Marekani ilivyoshirikiana na genge hilo la ukufurishaji nchini Iraq.
Sehemu moja ya nyaraka hizo inafichua kuwa, ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya A330 ilitua katika uwanja wa ndege wa Mosul wakati mji huo ulikuwa chini ya udhibiti wa Daesh, ambapo makamanda wa jeshi la Marekani waliteremka pamoja na kuteremsha silaha na zana nyingine za kijeshi.
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani ililikabidhi genge hilo silaha za kivita kama walivyokuwa wamekubaliana huko nyuma, na kisha kufanya mazungumzo na viongozi wa Daesh kwa muda wa masaa matatu na dakika 23 kabla ya wao kupanda ndege tena na kuondoka mjini Mosul, Iraq.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa, wakati ambapo makamanda wakuu wa ISIS walikamatwa katika miezi ya hivi karibuni, US iliutumia Umoja wa Mataifa kuwahamishia magaidi hao kaskazini mwa Afghanistan, Libya na kusini mwa Yemen, chini ya kisingizio cha 'usitishaji vita wa muda' huko Mosul.