Uhusiano wa kijeshi wa Iran na Oman wazidi kuimarika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i44076-uhusiano_wa_kijeshi_wa_iran_na_oman_wazidi_kuimarika
Kikao cha 14 cha Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiulinzi wa Oman na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeanza leo hapa mjini Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2018 03:24 UTC
  • Kikao cha Kamati ya Pamoja ya Kijeshi na Ulinzi ya Iran na Oman
    Kikao cha Kamati ya Pamoja ya Kijeshi na Ulinzi ya Iran na Oman

Kikao cha 14 cha Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiulinzi wa Oman na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeanza leo hapa mjini Tehran.

Ufunguzi wa kikao hicho cha siku tano umeongozwa kwa pamoja na Brigedia Jenerali Ghadir Nezami, Naibu wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Kimataifa na Brigedia Hamad bin Rashid al Balushi, Naibu wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Oman Operesheni na Mipango na pande mbili zimejadiliana njia za kustawisha ushirikiano wao katika masuala ya ulinzi.

Brigedia Jenerali Ghadir Nezami, Naibu wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Pande hizo mbili zimetilia mkazo njia za kuimarisha ushirikiano wao wa kijeshi hasa kwa kuzingatia nafasi ya kipekee ya Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi katika uchumi wa baharini na kiwango kikubwa cha meli za biashara na za mafuta zinazohitajia ushirikiano wa nchi za eneo hili wa kulinda usalama wa safari za vyombo hivyo vya baharini.

Iran na ndugu zao wa Oman wamekubaliana pia kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi yatakayohusiana na uokoaji na kutoa misaada. Mazoezi hayo ya pamoja yanatarajiwa kufanyika mwaka huu katika maji ya Ghuba ya Uajemi kwa uenyeji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ujumbe huo wa ngazi za juu wa kijeshi wa Oman unatarajiwa pia kufanya mazungumzo na maafisa wengine wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ziara yao hii humu nchini.