Apr 05, 2016 14:10 UTC
  • Zarif: Iran iko tayari kusaidia kutatua mgogoro wa Karabakh

Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Javad Zarif amesema Iran iko tayari kusaidia kurejesha utulivu katika eneo la Nagorno-Karabakh ambalo katika siku za karibuni limekuwa uwanja wa mapigano makali kati ya vikosi vinavyoungwa mkono na Armenia na vile vya serikali ya Azerbaijan.

Dakta Zarif ameyasema hayo leo katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia Edward Nalbandian, baada ya mazungumzo ya pande tatu aliyofanya hapo kabla na Waziri wa Mambo ya Nje wa Azerbaijan, Elmar Mammadyarov na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu.

"Lengo letu ni kuhatimisha mapigano", amesema Waziri Zarif na kutoa wito kwa nchi za eneo kusaidia kurejesha amani katika eneo la Karabakh.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi nzuri ya kusuluhisha mgogoro wa Karabakh kutokana na uhusiano mzuri ilionao na majirani zake wote hao wawili wa Armenia na Azerbaijan.

Watu wapatao 46 wameuawa katika mapigano ya siku tatu katika eneo lenye mgogoro la Nagorno-Karabakh.

Mnamo mwaka 1998, Waarmenia waishio katika eneo la Karabakh ambalo linatambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni sehemu ya ardhi ya Azerbaijan walijitenga na nchi hiyo na kujitangaza kuwa ni Jamhuri, hatua ambayo ilichochea vita vilivyosababisha vifo vya watu wapatao 30,000 hadi vilipokomeshwa kwa usitishaji mapigano mnamo mwaka 1994.

Wakati huohuo Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan imethibitisha leo kuwa makubaliano ya usitishaji vita katika eneo la Nagorno-Karabakh yamefikiwa kati ya nchi hiyo na waasi wanaoungwa mkono na Armenia.../

Tags