Jeshi la SEPAH la Iran lasambaratisha makundi mawili ya kigaidi mjini Tehran
(last modified Tue, 29 May 2018 08:02:44 GMT )
May 29, 2018 08:02 UTC
  • Jeshi la SEPAH la Iran lasambaratisha makundi mawili ya kigaidi mjini Tehran

Kamanda wa Kikosi cha Muhammad Rasulullah cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH, ametangaza kusambaratishwa makundi mawili ya kigaidi mjini Tehran.

Mohammad Reza Yazdi aliyasema hayo jana usiku katika marasimu ya uratibu ya mwaka wa 29 tangu kufariki dunia Imamu Ruhullah Khomein (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambayo pia yalihudhuriwa na waandishi wa habari na kusema, wanachama hao wa makundi mawili ya kigaidi walikuwa wamepanga kuibua machafuko na ghasia katika marasimu hayo.

Wanachama wa makundi ya kigaidi wenye idiolojia za Uwahabi

Kadhalika Kamanda Reza Yazdi amesisitiza kwamba, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH, limejiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa taifa hili na kwamba hatua yao yoyote itakabiliwa na radiamali kali. Sambamba na kubainisha kwamba hatua zote za kiusalama kwa ajili ya kuwawezesha wafanya ziara kutekeleza shughuili zao kwa amani kwenye marasimu  hayo zimechukuliwa amesema kuwa, uadui wa maadui wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran hauna mpaka wala ukomo na kwa ajili hiyo maandalizi yote ya kiusalama na kiulinzi yamekamilika kwa ajili ya kuhakikisha kumbukumbu hizo zinafanyika kwa amani.

Imam Ruhullah Khomein (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Kumbukumbu za kufariki dunia Imamu Ruhullah Khomein (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hufanyika tarehe 14 Khordad sawa na tarehe nne Juni. Kwa mnasaba huo maelfu ya wafanya ziara kutoka ndani na nje ya Iran hufika kwenye kaburi la Imamu Khomein kwa ajili ya kufanya ziara na kumuenzi mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.