Salami: Iran katu haitasitisha ustawi wa makombora
Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, Brigedia Jenerali Hussein Salami amepuuzilia mbali uwezekano wa Iran kufanya mazungumzo kuhusu kupunguza uwezo wake wa makombora.
Brigedia Jenerali Salami amesema Iran itazidi kuimarisha uwezo wake wa makombora na kuongeza kuwa, 'yeyote anayeogopa makombora ya Iran basi atafute hifadhi.' Jenerali Salami ametoa kauli hiyo akijibu matamshi ya hivi karibuni dhidi ya Iran yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo.
Naibu Kamanda wa IRGC amesema hatua ya Pompeo kuiomba Iran isitishe harakati zake katika eneo ni ishara kuwa Marekani haina uwezo wa kuizuia Iran. Brigedia Jenerali Salami pia amesema kauli ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ya kuitaka Iran isitishe uimarishaji wa makombora yake ya balistiki ina maana kuwa Marekani yenyewe haiwezi kuizuia Iran katika uga huo.
Brigedia Jenerali Salami amesema madola ya Magharibi hayakudhani kuwa Iran ingeweza kueneza ushawishi nje ya mipaka yake na kutishia satwa ya kibeberu ya madola hayo.
Katika hotuba aliyotoa Mei 21 mjini Washington, Pompeo alitaka Iran itakeleze maamrisho ya Marekani la sivyo itaangamizwa. Matamshi hayo yaliyojaa kiburi yamekosolewa vikali huku maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakisisitiza kuwa nchi hii itaendelea kufuata mkondo wake iliojiainishia.