Zarif: Sera za kigeni za Marekani zimekumbwa na mgogoro
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika makala yenye anwani inayosema: "Sera za Kigeni za Marekani Katika Mgogoro" ameandika: "Mapatano ya nyuklia ya Iran (JCPOA) yalikuwa mapatano ya tatu ya kimataifa Marekani kujiondoa baada ya kujiondoa katika mapatano ya kibiashara ya Bahari ya Pasifiki na mapatano ya tabianchi ya Paris."
Katika makala ambayo imechapishwa leo asubuhi katika magazeti ya Iran Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebaini kuwa: "Serikali ya sasa ya Marekani, kwa hatua zake, imehatarisha mapatano mengine ya kimataifa kama NAFTA, mfumo wa biashara huru na sehemu ya mfumo wa umoja wa mataifa." Ameongeza kuwa hatua hizo za Marekani zimetoa pigo kwa mfumo wa ushirikiano wa mataifa ya dunia na kudidimiza matumaini ya utatuzi wa kidiplomasia wa matatizo muhimu ya dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kuandika kuwa: "Kujitoa Marekani katika JCPOA pamoja na hatua yake ya upande mmoja ya kurejesha vikwazo vya nyuklia vilivyo kinyume cha sheria ni kilele cha kutotekeleza ahadi na ni ukiukaji mapatano hayo katika hali ambayo, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA, ambayo ni taasisi pekee ya kitaalamu husika, imesisitiza mara kadhaa katika ripoti zake kuwa, Iran imefungamana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA."
Zarif aidha amesisitiza kuwa: "Hivi karibuni, mnamo Mei 21 2018, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitoa hotuba isiyo na msingi, yenye lugha ya vitisho na yenye kuivunjia heshima Iran na kwa hakika huo ni ukiukaji wa wazi wa taratibu zinazotambulika kimataifa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: "Masharti 12 ambayo (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani) Mike Pompeo aliyataja ni ya kichekesho kwani Marekani inazidi kutengwa kimataifa kutokana na sera zake za kudhoofisha udiplomasia na mfumo wa ushirikiano wa pande kadhaa."
Zarif amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anapaswa kufahamu kuwa, katika kipindi cha miongo minne, wananchi wa Iran wamekabiliana na hujuma pamoja na mashinikizo mbali mbali ya Marekani ikiwa ni pamoja na njama za kuuangusha mfumo wa Kiislamu, kuihujumu nchi hii kijeshi, kunga mkono mvamizi katika vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, kuiwekea nchi hii vikwazo vya upande mmoja na hata kuitungua ndege ya abiria ya nchi hii."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nguzo kubwa zaidi ya kisiasa ya mfumo wa kisiasa nchini Iran ni wananchi ambao wanataka uhusiano na dunia kwa msingi wa kuheshimiana. Hali kadhalika Zarif ameashiria hatua zilizo kinyume cha sheria za Marekani kuhusu Quds Tukufu (Jerusalem) na kusema kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni hasa katika Ukanda wa Ghaza na Syria ni sehemu ya sera zisizo sahihi za Marekani.