Kiongozi: Maadui watafeli tena katika njama zao dhidi ya Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia njama za maadui ambao wanalenga kuibua ufa baina ya mfumo wa Kiislamu Iran na wananchi na kusema: "Iwapo misingi ya nguvu za kitaifa itaimarishwa na kusiwepo na udhaifu na kusalimu amri mbele ya adui, basi wanaolitakia taifa hili mabaya watafeli tena katika malengo yao."
Ayatullah Ali Khamenei, ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mahalafi ya kuhitimu maafisa wa jeshi katika Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS. Ameongeza kuwa: "Ushahidi mkubwa zaidi kuwa taifa la Iran limepata nguvu ni kuwa, moja ya madola katili na yenye kumwaga damu zaidi duniani, yaani Marekani, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita imekuwa ikifanya kila iwezalo kukabiliana na Iran lakini haijaweza kufanya lolote, na katika upande wa pili Iran imeweza kustawi zaidi."
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Marekani imezidisha uhasama wake kutokana na ustawi na maendeleo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na tabaan taifa la Iran nalo linaendelea kuichukia Marekani."
Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfumo unaowategemea wananchi, imani na mahaba yao. Ameashiria kufeli jitihada na njama za marais waliotangulia wa Marekani za kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: "Lengo la mashinikizo ya sasa ya kiuchumi ni kuwafanya watu wachoke na wapoteza matumaini, lakini kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, mshikamano wetu na wananchi utazidi kuimarika na kwa kudumisha mshikamano wenye kumvunja adui, tutaweza kuwaimarisha vijana waumini, wenye ari na wenye harakati."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nguvu halisi ni zile zinazotoka ndani ya taifa na zina msingi wa uhuru na kujitegemea. Ameongeza kuwa: "Haiwezi kutajwa nguvu pale baadhi ya nchi zinapowapa maajinabi pesa na kununua silaha za kigeni na kuziweka katika maghala pasina hata kujua kuzitumia, au kuleta majeshi kutoka maeneo ya mbali ya dunia yaje kuweka kambi katika nchi zao na kunyonya damu ya taifa ili kubakisha hai na kulinda utawala wa ukoo; huu ni mfano wa ujinga na udhalili."
Ayatullah Khamenei amesema sababu nyingine inayoashiria uwezo na nguvu kubwa za Iran ni kuwa, Marekani imeunda miungano ya kieneo kwa lengo tu la kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislalmu. Ameendelea kusema kuwa, iwapo Marekani ingeweza kufikia malengo yake bila msaada basi haingehitaji kuunda muungano na madola yaliyodhalilika na yanayopinga mageuzi katika eneo."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesisitiza kuwa: "Katika muda usio mrefu, taifa la Iran litapata hadhi ambayo itamzuia adui hata thubutu kutekeleza hujuma ya kijeshi, kiuchumi, kiusalama na kisiasa dhidi yake na vijana watashuhudia siku hiyo."