Hatami: Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i47085-hatami_iran_haitasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo_ya_maadui
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii katu haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui na itavuka salama kipindi hiki cha sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2018 20:52 UTC
  • Hatami: Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii katu haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui na itavuka salama kipindi hiki cha sasa.

Brigedia Jenerali Amir Hatami aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkoa wa Zanjan, kaskazini magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, bila kuona haya hata kidogo, adui anakiuka ahadi na mapatano yote na kisha anachukua hatua za kuiwekea Iran vikwazo. Ameongeza kuwa: "Watu wa Iran wana historia ndefu ya kuwa na heshima na nguvu na pia maelfu ya Wairani wameuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa kwa ajili ya kulinda Mapinduzi ya Kiislamu na hivyo hakuna shaaka nchi hii itaweza pia kuvuka kipindi hiki."

Brigedia Jenerali Hatamu amebainisha kuwa, vikwazo vya maadui dhidi ya Iran ni fursa nzuri ambayo inapaswa kutumiwa kuimarisha uwezo wa nchi.

Hivi karibuni Brian Hook, mkurugenzi wa sera katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alifafanua sera mpya ya utawala wa Donald Trump kuhusu Iran na kutangaza kuwa: "Duru mpya ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran itajumuisha sekta za utengenezaji magari na dhahabu na itaanza Agosti 4. Duru nyingine ya vikwazo itakuwa katika sekta za nishati na mabadilishano ya kifedha ya benki za Iran na itaanza kutekelezwa Novemba nne.