Iran yalaani kuendelea jinai za wavamizi Wasaudi dhidi ya watu wa Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuendelea jina za kila siku za wavamizi Wasaudi na kimya cha jamii ya kimataifa kumepelekea hali ya watu wa Yemen kuwa mbaya zaidi.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo Ijumaa katika taarifa ya kulaani hujuma ya ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya hospitali na soko katika Bandari ya Al Hudaydah ambapo makumi ya watu wameuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa. Kati ya raia wasio na hatia waliopoteza maisha katika jinai hiyo mpya ya kivita ya Saudi Arabia ni wanawake na watoto wachanga. Qassemi amesema mauaji hayo ni mwendelezo wa maangamizi ya kimbari na jinai za kuogofya za Saudia na waitifaki wake dhidi ya taifa la Yemen.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kulenga maeneo ya kiraia kama vile mashospitali, nyumba za makazi raia na maeneo ya umma kunafanywa na Saudia na waitifaki wake kama njia ya kufidia kufeli na kushindwa kwao katika medani ya vita. Ameongeza kuwa mashambulizi hayo ya Saudia dhidi ya hospitali na soko katika Bandari ya Al Hudaydah ni jinai ya kivita.
Qassemi ameendelea kusema kuwa, kuwadondoshea mabomu raia wa Yemen kila siku na kuua watu wasio na hatia wala ulinzi kunakofanywa na ndege za kivita za Saudia na Imarati hakupaswi kuwa jambo la kawaida katika fikra za umma katika eneo la Mashariki ya Kati na katika uga wa kimataifa kwani hali kama hiyo itayafanya maafa ya Wayemen kuwa mabaya zaidi.
Alasiri ya jana Alhamisi, ndege za kivita za Saudia zilidondosha mabomu katika Hospitali ya Al Thaura na soko la samaki katika mji wa bandarani wa Al Hudaydah magharibi mwa Yemen na katika jinai hiyo idadi ya waliofariki dunia hadi sasa ni zaidi ya 60 huku wengine wasiopungua 120 wakijeruhiwa vibaya.