IRGC: Kipigo cha Iran dhidi ya magaidi Kurdistan kimetuma ujumbe kwa maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48114-irgc_kipigo_cha_iran_dhidi_ya_magaidi_kurdistan_kimetuma_ujumbe_kwa_maadui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema jibu kali lilitolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kuvurumisha makombora dhidi ya magaidi katika eneo linalojiendeshea mambo yake la Kurdistan nchini Iraq lilituma ujumbe wa wazi na wenye maana kwa maadui wanaodhani kuwa wanaweza kuihujumu Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2018 09:30 UTC
  • IRGC: Kipigo cha Iran dhidi ya magaidi Kurdistan kimetuma ujumbe kwa maadui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema jibu kali lilitolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kuvurumisha makombora dhidi ya magaidi katika eneo linalojiendeshea mambo yake la Kurdistan nchini Iraq lilituma ujumbe wa wazi na wenye maana kwa maadui wanaodhani kuwa wanaweza kuihujumu Iran.

Meja Jenerali Mohammad Ali Jaafari amesema hayo leo Alkhamisi katika mazishi ya mashahidi 135 mjini Tehran na kubainisha kuwa, hatua ya Iran ya kujibu mapigo dhidi ya chokochoko za magenge ya kigaidi katika eneo la Kurdistan ni onyo kwa maadui wa taifa hili hususan nchi za kibeberu zinazodhani kuwa zinaweza kuidhalilisha na kula njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kamanda Mkuu wa SEPAH amesema, maadui wanaelewa fika kwamba hawawezi kivyovyote vile kuiteteresha kiulinzi Iran na wanatambua uwezo mkubwa wa kiulinzi wa taifa hili na kuongeza kwamba, "Makombora yetu yanaweza kulenga maadui walioko hadi umbali wa kilomita 2,000 kwa usahihi mkubwa."

 

Sehemu ndogo ya makombora ya Iran ya S-300

Kauli hii ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran inakuja siku mbili baada ya Kamanda wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri kusisitiza kuwa taifa la Iran lina haki ya kujilinda na kwamba chokochoko za maadui zitakabiliwa na jibu kali zaidi kutoka Iran. 

Jumamosi iliyopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilijibu hujuma za magaidi hao wa Kurdistan kwa kuvurumisha makombora saba ya masafa mafupi dhidi ya mkusanyiko wa makamanda wa kigaidi katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.