Uganda na Iran kuimarisha ushirikiano katika uga wa sayansi na teknolojia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48598-uganda_na_iran_kuimarisha_ushirikiano_katika_uga_wa_sayansi_na_teknolojia
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Uganda ametoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa sayansi na teknolojia.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 05, 2018 12:08 UTC
  • Uganda na Iran kuimarisha ushirikiano katika uga wa sayansi na teknolojia

Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Uganda ametoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa sayansi na teknolojia.

Elioda Tumwesigye ametoa mwito huo leo Ijumaa mjini Kampala katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya elimu na teknolojia, Sorena Sattari ambaye yuko katika safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika Mashariki.

Amesema serikali ya Kampala ipo tayari kuandaa mazingira ya kuanzishwa kampuni za Iran nchini humo, ambazo zitafanikisha uzalishaji wa bidhaa za teknolojia kwa ushirikiano na Uganda katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Katika mazungumzo hayo, Sattari mbali na kuashiria uwezo mkubwa wa Iran katika nyuga za sayansi na teknolojia kama vile teknolojia ya nano na bioteknolojia, pamoja na uzoefu wa Iran wa kujitosheleza katika uzalishaji wa madawa, amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili  ili kuandaa mazingira ya kuimarisha mabadilishano ya bidhaa na huduma za kiteknolojia za nchi mbili hizo.

Bendera za Iran na Uganda

Hapo jana, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya elimu na teknolojia alikutana na kufanya mazungumzo mjini Nairobi na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Kenya, Peter Munya na kusisitiza juu ya kustawishwa usafirishwaji nje bidhaa za teknolojia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, kuimarisha uhusiano wake na nchi za bara la Afrika ni katika sera zake kuu za mambo ya nje.