"Makombora, jibu na ujumbe wa Iran kwa waungaji mkono wa ugaidi"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48600-makombora_jibu_na_ujumbe_wa_iran_kwa_waungaji_mkono_wa_ugaidi
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran sanjari na kupongeza mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC dhidi ya ngome za magaidi nchini Syria amesema operesheni hiyo ilikuwa jibu la Iran lililobeba ujumbe mahsusi kwa magaidi, wafadhili na waungaji mkono wao.
(last modified 2026-02-26T05:06:13+00:00 )
Oct 05, 2018 15:45 UTC

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran sanjari na kupongeza mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC dhidi ya ngome za magaidi nchini Syria amesema operesheni hiyo ilikuwa jibu la Iran lililobeba ujumbe mahsusi kwa magaidi, wafadhili na waungaji mkono wao.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi amesema bila shaka mashambulizi hayo yaliyatanabahisha magenge ya kigaidi kuhusu uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu wa kujihami na hata kulidhaminia usalama eneo hili la Mashariki ya Kati.

Amesema, "Makombora yetu yalivurumishwa kutoka umbali wa zaidi ya kilomita 500 na yakafanikiwa kuwaangamiza magaidi wasiopungua 40 wakiwemo makamanda wao, mbele ya macho ya Marekani."

Ayatullah Siddiqi amesisitiza kuwa, mashambulizi hayo ya Sepah ni onyo na indhari kwa wafadhili wa ugaidi juu ya matokeo mabaya ya njama zao.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran siku chache zilizopita, liliyashambulia makao ya viongozi wa jinai za kigaidi mashariki mwa Furat nchini Syria ambao walihusika na mauaji ya kigaidi ya karibuni katika mji wa Ahvaz kusini magharibii mwa Iran. 

Ngome za magaidi zilizopigwa na makombora ya Iran huko Syria

Itakumbukwa kuwa, mamluki wa makundi ya kitakfiri ya al Ahvazia na Daesh ambayo yanaungwa mkono na serikali za Uingereza na Saudi Arabia tarehe 22 Septemba waliwashambulia askari wa ulinzi wa Iran waliokuwa katika gwaride katika mji wa Ahvaz katika maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu na kuuwa shahidi watu 25 na kujeruhi makumi ya wengine. 

Kwengineko katika hotuba yake, Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi ametoa radiamali yake kwa matamshi yaliyo dhidi ya Iran yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani na kusema kuwa, taifa la Iran kwa mara nyingine tena litatoa jibu kali kwa watawala wa Washington.