Zarif: Mossad inatekeleza njama za kuvuruga uhusiano wa Iran na EU
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49172-zarif_mossad_inatekeleza_njama_za_kuvuruga_uhusiano_wa_iran_na_eu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madai ya Denmark dhidi ya Iran ni katika fremu ya oparesheni ya upotoshaji inayotekelezwa na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel linalojulikana kama Mossad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2018 03:16 UTC
  • Zarif: Mossad inatekeleza njama za kuvuruga uhusiano wa Iran na EU

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madai ya Denmark dhidi ya Iran ni katika fremu ya oparesheni ya upotoshaji inayotekelezwa na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel linalojulikana kama Mossad.

Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, mapema leo asubuhi, Zarif amesema hatua ya Mossad ya kueneza hadaa na upotoshaji wa makusudi itazidi kuimarisha azma ya Iran ya kuwa na uhusiano mzuri na dunia.

Jana Jumatano pia, Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema Marekani, Utawala wa Kizayuni wa Israel na wengine ambao leo wanakabiliwa na tuhuma nzito, wanajaribu kutekeleza vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa lengo la kuvuruga uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya. Ameongeza kuwa njama hizo zinatekelezwa wakati huu wa kukaribia duru mpya ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Kuhusiana na kadhia hiyo, jana Jumatano gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limekiri kuwa, Israel imehusika moja kwa moja katika kuvuruga uhusiano wa Iran na Denmark. Gazeti hilo limeandika kuwa, Mossad ilikuwa na usahidi wa eti mpango wa Iran wa kutekeleza oparesheni nchini Denmark na imeikabidhi Copenhagen taarifa hizo.

Siku ya Jumanne,  Denmark ilijiunga na msururu wa baadhi ya nchi za Ulaya zinazotoa tuhuma dhidi ya Iran na kudai kuwa eti Iran ilikuwa inapanga kutekeleza oparesheni ya mauaji nchini humo na kwa msingi huo ilimuita balozi wa Iran mjini Copenhagen kulalamikia suala hilo.