Salehi: Uwezo wa makombora wa Iran umeiduwaza dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49453-salehi_uwezo_wa_makombora_wa_iran_umeiduwaza_dunia
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi amesema mafanikio ya Iran katika uzalishaji wa makombora umeishangaza dunia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 12, 2018 04:32 UTC
  • Salehi: Uwezo wa makombora wa Iran umeiduwaza dunia

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi amesema mafanikio ya Iran katika uzalishaji wa makombora umeishangaza dunia.

Salehi aliyasema hayo jana Jumapili katika Maonyesho ya Mafanikio ya Iran katika Uga wa Makombora na Nyuklia mjini Qazvin na kubainisha kuwa, uwezo huo mkubwa wa Iran wa kuimarisha mifumo yake ya kujihami haswa uzalishaji wa makombora na mradi wa nyuklia wenye malengo ya amani licha ya kukabiliwa na vikwazo, ni jambo ambalo limewawacha walimwengu vinywa wazi.

Ameongeza kuwa, vikwazo haviwezi kulizuia taifa hili kupiga hatua kwa kuwa taifa hili limekuwa chini ya vikwazo hivyo vya kidhalimu tangu mwanzoni mwa vuguvugu la Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, na kwamba sera ya vikwazo ya Marekani sio kitu kipya hapa nchini.

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua kuwa, "Hivi sasa, miaka 40 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran inajivunia kupata mafanikio chungu nzima katika nyuga mbalimbali licha ya vikwazo, mashinikizo, vizingiti na vita vya miaka minane vya kulazimishwa na Iraq, na jambo hili bila shaka limeyaduwaza madola ya kibeberu na maadui wa taifa hili."

Makombora ya Iran yaliyohifadhiwa chini ya ardhi

Wiki iliyopita, vikosi vya Jeshi la Iran vilifanyia majaribio kwa mafanikio mifumo kadhaa ya ulinzi wa anga, sambamba na kuzindua makombora ya kizazi kipya ya Sayyad 2, na mfumo wa makombora wa ‘Talash’ uliozalishwa na wataalamu wa hapa nchini, wenye uwezo wa kutungua makombora umbali wa kilomita 150 na katika anga za mbali.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora, na kwamba uwezo huo unaashiria nguvu, heshima, uhuru na kujiamini taifa hili.