IAEA yasisitiza tena kuwa Iran imefungamana na JCPOA
Kwa mara nyingine tena, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umethibitisha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu na ahadi zake zote chini ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukia Amano katika hotuba yake mbele ya Bodi ya Wanachama wa wakala huo na kusisitiza kwamba, Iran inaendelea kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano hayo ya nyuklia.
Amano ameashiria ripoti ya wakala huo iliyosambaziwa nchi wanachama wa IAEA mapema mwezi huu na kubainisha kuwa, Iran ingali inaendelea kutekeleza na kufungamana na majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.
Amano ameiasa Iran iendelee kushirikiana kikamilifu na wakaguzi wa IAEA kukagua vituo vyake vya nyuklia.
Ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zimekuwa zikisisitiza kuwa Iran imetekeleza na kuheshimu vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyotiwa saini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kundi la 5+1 Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.
Licha ya ripoti hizo zinazotolewa mara kwa mara na IAEA, lakini Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 Mei mwaka huu aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano hayo ya JCPOA, na kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Tehran, suala ambalo limekabiliwa na upinzani mkubwa wa nchi nyingine zilizoyatia saini.