Nov 24, 2018 02:46 UTC
  • Kikao cha Tehran chalaani kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel

Taarifa ya mwisho ya kikao cha "Nafasi ya Vyama na Wanaharakati wa Kisiasa katika Kupunguza Hitilafu za Kimadhehebu na Kulinda Malengo ya Palestina" kilichofanyika hapa mjini Tehran imelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na imesisitizia udharura wa kulindwa Quds na Palestina kwa nguvu zote.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, washiriki wa kikao hicho cha jana Ijumaa wamehimiza kuweko umoja na mshikamano wa vyama vya nchi za Kiislamu kama sehemu ya juhudi za kuleta umoja na mshikamano katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na pia kuutia nguvu msingi wa kifikra na kisiasa wa Waislamu ili kuipa ushindi kambi ya muqawama.

Taarifa hiyo ya mwisho ya kikao hicho imesisitizia pia wajibu wa kupunguzwa mivutano ya kimadhehebu na misimamo mikali ya kidini sambamba na kutiwa nguvu mijadala na mazungumzo ya kisiasa kuhusu kadhia ya Palestina na muqawama.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho

 

Tamko hilo limeongeza kuwa, ni jambo la dharura kwa taasisi zote za kisiasa kuhisi ni jukumu lao kushughulikia vilivyo suala la Palestina na mhimili wa muqawama katika kupambana na moyo wa kibeberu wa Marekani na tabia ya kupenda vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Vilevile washiriki wa kikao hicho cha Tehran wameitaka Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu kuifungulia mashtaka Marekani kwa jinai zake za kuunda genge la kigaidi la Daesh (ISIS), kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na kuusaidia utawala wa kiimla wa Aal Saud unaofanya jinai za kila namna dhidi ya wananchi wa Yemen, ili vitendo hivyo vilaaniwe rasmi kimataifa na kulipwa fidia wahanga wote.

Tags