Zarif ajibu matamshi ya Pompeo, asema dawa ya moto ni moto
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50623-zarif_ajibu_matamshi_ya_pompeo_asema_dawa_ya_moto_ni_moto
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekadhibisha madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuhusu majaribio ya makombora na miradi ya masuala ya anga ya Iran.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jan 03, 2019 23:53 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekadhibisha madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuhusu majaribio ya makombora na miradi ya masuala ya anga ya Iran.

Muhammad Javad Zarif amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba: Kurushwa angani satalaiti ya masuala ya anga au kufanya majaribio ya makombora ya Iran hakukiuki azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bali Marekani ndiyo iliyokiuka azimio hilo la Baraza la Usalama.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema Marekani haina hadhi ya kuzungumzia majaribio ya makombora ya Iran na amewakumbusha maafisa wa nchi hiyo kwamba, vitisho hukabiliwa na vitisho, na heshima hufuatiwa na heshima. 

Alkhamisi ya jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alidai kuwa, maroketi ya Iran ya kutuma satalaiti katika anga za mbali yanatumia teknolojia inayoshabihiana na ile ya makombora yanayoweza kuvuka mabara, na kwamba Iran haipaswi kuwa na miradi ya kutengeneza maroketi ya kutuma satalaiti katika anga za mbali.

Mike Pompeo

Bila ya kutoa ushahidi wowote, Pompe amedai kuwa, kurusha satalaiti katika anga za mbali kunakinzana na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa!

Ni vyema kuashiria hapa kwamba, madai hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani yametolewa katika hali ambayo hadi sasa Baraza la Usalama halijawahi kutoa hata taarifa moja kuhusu miradi ya Iran ya kurusha satalaiti katika anga za mbali. Vilevile Russia na nchi za Ulaya zimepinga madai hayo ya Marekani.