Baqeri: Vitisho havitaishurutisha Iran ifanye mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51408-baqeri_vitisho_havitaishurutisha_iran_ifanye_mazungumzo_kuhusu_uwezo_wake_wa_makombora
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vitisho vya adui haviwezi kuifanya Iran isalimu amri na kusitisha jitihada zake za kustawisha uwezo wake wa makombora.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 07, 2019 22:38 UTC
  • Baqeri: Vitisho havitaishurutisha Iran ifanye mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vitisho vya adui haviwezi kuifanya Iran isalimu amri na kusitisha jitihada zake za kustawisha uwezo wake wa makombora.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri alisema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran katika Maonyesho ya Mafanikio ya Kiulinzi ya Iran na kufafanua kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimefanikiwa kuzalisha asilimia 80 ya suhula na zana zinazohitajika ili kuimarisha makombora yake na kuzalisha silaha zinazohitajika, zikiwemo za nchi kavu, baharini na angani kwa shabaha ya kujihama kutokana na chokochoko za maadui.

Amesema makelele ya maadui na vitisho vyao katu havitaishurutisha Iran ifanye mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora.

Zana za kijeshi za Iran

Huku akiashiria namna vyombo vya usalama vya Iran ya Kiislamu vilivyofanikiwa kuzima njama za maadui na magenge ya kigaidi ambayo yamekuwa yakijaribu kujipenyeza humo nchini ili kuvuruga usalama wa taifa, Meja Jenerali Baqeri amesema kuwa, wataalamu wa kijeshi wa Iran wana uwezo wa hali ya juu katika kukidhi mahitaji ya kiulinzi ya taifa hili.

Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa, itakubali kufanya mazungumzo kuhusu makombora ya Iran iwapo tu Marekani na nchi za Ulaya zitaangamiza kwanza silaha zao za nyuklia na makombora yao masafa marefu. 

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri ameongeza kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko tayari kubadilishana tajriba na uzoefu wake wa kijeshi na nchi ndugu na za Kiislamu ili kupiga jeki jithada zao za kupambana na ugaidi.