Mkutano wa Warsaw, jitihada zilizofeli za Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51539-mkutano_wa_warsaw_jitihada_zilizofeli_za_marekani_dhidi_ya_iran
Katika fremu ya mtazamo wake kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati, Marekani jana ilifungua mkutano wa siku mbili katika mji mkuu wa Poland, Warsaw uliopewa jina la "Amani na Usalama wa Mashariki ya Kati. Washington inasema nchi 70 zimealikwa kushiriki katika mkutano huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2019 03:47 UTC
  • Mkutano wa Warsaw, jitihada zilizofeli za Marekani dhidi ya Iran

Katika fremu ya mtazamo wake kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati, Marekani jana ilifungua mkutano wa siku mbili katika mji mkuu wa Poland, Warsaw uliopewa jina la "Amani na Usalama wa Mashariki ya Kati. Washington inasema nchi 70 zimealikwa kushiriki katika mkutano huo.

Hata hivyo kinyume na madai ya Marekani inayosema mawaziri wa mambo ya nje wa makumi ya nchi wanahudhuria mkutano wa Warsaw, nchi nyingi zimetangaza kuwa hazitashiriki katika mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema mwanzoni mwa mkutano huo kwamba, lengo lake ni eti kuimarisha amani na uhuru katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kumulika zaidi satuwa na ushawishi wa Iran katika eneo hilo. Pompeo amesema: Mkutano huu umejikita zaidi juu ya Iran. 

Wamarekani wanadhani kwamba, mkutano huo utaweza kuunda aina fulani ya muungano wa kimataifa dhidi ya Iran kwa kukusanya pamoja nchi kadhaa za dunia. Lengo kuu la Marekani ni kutaka kuufanya mkutano huo kuwa anga ya propaganda chafu dhidi ya ushawishi wa Iran eneo la Mashariki ya Kati. Hata hivyo msimamo hasi wa nchi wanachama katika kundi la 4+1 yaani Russia, Ufaransa, Uingereza, China na Ujerumani kuhusiana na mkutano wa Warsaw unaonesha kuwa, Washington inakabiliwa na visingiti vingi katika njia ya kufikia malengo yake. Russia kama nchi yenye taathira kubwa katika masuala ya Mashariki ya Kati, imetangaza waziwazi kwamba, inapinga mkutano wa Kimarekani wa Warsaw na kwamba lengo lake ni kutaka kukwamisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Nchi kubwa za Ulaya pia zimetuma jumbe za ngazi za chini katika mkutano huo. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani, Heiko Maas ametangaza kuwa hatashiriki katika mkutano uliodhidi ya Iran wa Warsaw na kwamba afisa mmoja wa wizara hiyo atahudhuria vikao vyake. 

Awali maafisa wa baadhi ya nchi za Ulaya akiwemo Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini walikuwa tayari wametangaza kuwa, hawatashiriki katika mkutano huo. 

Mike Pompeo

Kutoshiriki mawaziri wa baadhi ya nchi za Ulaya katika mkutano wa Warsaw ni kielelezo cha kupanuka zaidi mpasuko baina ya Brussels na Washington; kwa msingi huo inaonekana kuwa, mkutano huo unafanyika katika mazingira ya mahusiano baridi ambayo yataizuia Marekani kutimiza malengo yake ya awali dhidi ya Iran.

Kuongezeka ukosoaji dhidi ya mielekeo ya kuipiga vita Iran ya mkutano huo kuliilazimisha Marekani ibadili ajenda na maudhui zake kabla ya kufanyika. Kinyume na tangazo la awali la Marekani kuhusu malengo mkutano huo, taarifa iliyotolewa karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ilisema kuwa, utajadili masuala kadhaa kama migogoro ya kikanda na taathira zake kwa raia, ustawishaji wa makombora na marufuku ya silaha, usalama wa mitandao ya kijamii na vitisho vipya katika sekta ya nishati na suala la kupambana na misimamo mikali.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, maafisa wa serikali ya Marekani wameamua kubadili ajenda na maudhui za mkutano wa Warsaw kutokana na kususiwa au kupewa uzito wa chini na nchi nyingi kubwa duniani kama Russia, na China. Wanasema hatua hiyo imechukuliwa ili Washington isikimbiwe na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nyingine.

Donald Trump na Mike Pompeo

Jambo jingine muhimu ni kwamba, mawaziri wa mambo ya nje na maafisa wa nchi ambazo zimeamua kushiriki mkutano wa Warsaw ni wa makundi yasiyokuwa na uwiano na yenye hitilafu kubwa ambayo ni vigumu sana kuweza kutimiza matakwa ya Marekani ya kutaka kuanzisha muungano eti wa kimataifa dhidi ya Iran. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Dakta Muhammad Javad Zarif siku chache zilizopita alindika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter akiiambia Poland na washiriki katika mkutano wa Warsaw kwamba: Wale wote walioshiriki katika mkutano uliopita wa Marekani dhidi ya Iran ama wamekufa au wamepoteza heshima na kufedheheka au wametimuliwa; na Iran imekuwa imara na yenye nguvu zaidi kuliko hapo awali."

Muhammad Javad Zarif

Iran inasisitiza kuwa mkutano huo hautakuwa na taathira yoyote katika siasa na misimamo yake kuhusu eneo la Mashariki ya Kati. Meja Jenerali Muhammad Baqiri ambaye ni Kamanda wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mkutano wa Warsaw hauna thamani yoyote na kwamba hautakuwa na taathira kwa kazi na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu.