Iran yalaani shambulizi la Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51725-iran_yalaani_shambulizi_la_wazayuni_dhidi_ya_msikiti_wa_al_aqsa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali hujuma iliyofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na maeneo mengine ya kihistoria na Kiislamu huko Baitul Muqaddas.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 22, 2019 14:36 UTC
  • Iran yalaani shambulizi la Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali hujuma iliyofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na maeneo mengine ya kihistoria na Kiislamu huko Baitul Muqaddas.

Bahram Qassemi amesema kuwa, mauaji na ukandamziaji wa kikaumu na kidini unaendelea kufanyika huko Baitul Muqaddas tangu Wazayuni walipovamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kimya cha kutisha cha baadhi ya nchi za eneo hili la Mashariki ya Kati mbele ya uvamizi na uhalifu unaoendelea kufanywa na Wazayuni na kushiriki kwao katika mchezo wa maonyeho wa Kimarekani na Kizayuni huko Warsaw nchini Poland na vilevile kuanzisha uhusiano wa wazi na wa siri na utawala unaofanya mauaji dhidi ya raia wa Palestina ndivyo vinavyowahamasisha na kuwatia kiburi Wazayuni cha kushambulia na kuyavunjia heshima maeneo ya kihistoria na ya Kiislamu ya Palestina. 

Askari wa Israel wamevunjia heshima Msikiti wa al Aqsa

Bahram Qassemi amepongeza mapambano ya watu wa Palestina hususan wakazi wa Baitul Muqaddas kwa ajili ya kulinda maeneo matakatifu ya mji huo na ametoa wito kwa nchi za Kiislamu na jumuiya za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kulaani na kuzuia uhalifu na hatua za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Siku chache zilizopita utawala wa Kizayuni wa Israel ulifunga Mlango wa Rahma ambao ni miongoni mwa milango ya kuingia katika Msikiti wa al Aqsa na kuzuia Waislamu kwenda kutekeleza ibada ya Swala. Hatua hiyo imezusha machafuko makubwa.