Feb 26, 2019 02:37 UTC
  •  Amir-Abdollahian: Marekani inataka kuzusha machafuko nchini Venezuela

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amelaani hatua ya Marekani ya kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela na kusema kuwa, Washington inataka kuiondoa madarakani serikali halali na kuitumbukiza nchi hiyo katika vurugu na machafuko.

Hossein Amir-Abdollahian, amesema hayo katika mazungumzo yake na Alexis Bandrich Vega, balozi wa Cuba hapa mjini Tehran ambapo ameashiria kushadidi hatua za chuki na uhasama za Marekani dhidi ya baadhi ya nchi za Amerika ya Latini na kuongeza kuwa, kufanyika mazungumzo ya kisiasa baina ya serikali halali na wapinzani nchini Venezuela ni utatuzi mwafaka kwa ajili ya kuzima njama za Marekani.

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa  amesema kuwa, daima Tehran imekuwa ikitetea mamlaka na haki ya kujitawala mataifa na kupinga uingiliaji wa kigeni wa aina yoyote ile katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza pia katika mazungumzo yake hayo na balozi wa Cuba hapa nchini juu ya azma ya kutaka kuimarishwa na kupanuliwa zaidi ushirikiano kati ya Tehran na Havana.

Kwa upande wake Alexis Bandrich Vega, balozi wa Cuba hapa mjini Tehran ameyataja Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama kigezo muhimu cha wapigania ukombozi ulimwenguni na kusema kuwa, nchi yake inataka kustawisha zaidi uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Balozi wa Cuba mjini Tehran amelaani pia uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela na kutangaza kuwa, serikali ya Havana inaiunga mkono serikali halali ya Rais Nicolas Maduro.

Tags