Igizo jengine la Pompeo la uenezaji hofu na chuki dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52466-igizo_jengine_la_pompeo_la_uenezaji_hofu_na_chuki_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ameifufua tena kampeni ya uenezaji hofu na chuki dhidi ya Iran kwa kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile alichodai, nafasi haribifu iliyonayo katika eneo la Magharibi ya Asia na kuunga mkono ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2019 00:05 UTC
  • Igizo jengine la Pompeo la uenezaji hofu na chuki dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ameifufua tena kampeni ya uenezaji hofu na chuki dhidi ya Iran kwa kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile alichodai, nafasi haribifu iliyonayo katika eneo la Magharibi ya Asia na kuunga mkono ugaidi.

Pompeo alizusha madai hayo siku ya Jumatano wakati akiwasilisha ripoti yake mbele ya kamati ya mambo ya nje ya Baraza la Wawakilishi la Marekani na kuongeza kwamba, Iran ingali inatumia suhula zake kueneza vita katika nchi za Iraq, Yemen na Syria na kwamba itafika mbali zaidi ya huko. Kisha waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani akadai kwamba, Wahouthi, hadi sasa wamefyatua na kudondosha makumi ya makombora yaliyotengezwa Iran ndani ya ardhi ya Saudi Arabia na kwamba Wasaudi wanachukua hatua za kujihami kwa kukabiliana na makombora hayo ya Wahouthi.

Pompeo akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Wawakilishi la Marekani

Msimamo huo na tuhuma hizo za waziri wa mambo ya nje wa Marekani dhidi ya Iran si mpya na wala hii haitakuwa mara ya mwisho kutolewa. Ili kufanikisha malengo na sera zao haramu katika eneo la Magharibi ya Asia, viongozi wa Marekani wenye misimamo ya kufurutu mpaka, siku zote wamekuwa wakiifanya Iran kisingizio cha kutetea kushindwa kwao katika eneo hili.

Mchango chanya na athirifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la kistratejia la Magharibi ya Asia, umekuwa kikwazo kikubwa kwa ufanikishwaji wa siasa za kikoloni za Marekani na waitifaki wake katika eneo hili. Mchango mkuu wa Iran katika kupambana na ugaidi katika nchi za Syria na Iraq, umevuruga na kufelisha mkakati uliokusudiwa kufanikishwa na Marekani ndani ya nchi hizo mbili, kwa kutumia chaka la uwepo wa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).

Trump akikiri hadharani kuhusika serikali ya Marekani katika kuasisi DAESH (ISIS)

Iran imezisaidia Iraq na Syria katika kupambana na ugaidi kutokana na ombi la serikali za nchi hizo; na ushirikiano wao wa pamoja uliifanya 'khilafa' bandia liliyojitangazia kundi la ukufurishaji la Daesh katika nchi za Syria na Iraq ibaki kuwa ndoto za alinacha. Mchango chanya na athirifu wa Iran katika kupambana na ugaidi, ulifichua na kudhihirisha nia chafu na halisi ya Magharibi na hasa Marekani kuhusiana na baa la ugaidi. Tukiuhakiki mtazamo wa kizandiki na kindumakuwili wa Marekani kuhusu ugaidi, ndipo tutakapoweza kufahamu chanzo hasa cha madai ya viongozi wa Marekani dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa duru mbali mbali, Marekani imehusika na imechangia katika uundwaji wa Daesh nchini Iraq na baadaye katika uwepo wa kundi hilo la kitakfiri ndani ya ardhi ya Syria. Kuhusiana na suala hilo, hivi karibuni, veterani mmoja wa vita nchini Marekani ameandika barua ya wazi, akiweka hadharani mengi yaliyofichikana kuhusu misaada iliyotolewa na Marekani katika kufanikisha uundaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo hili la Asia Magharibi.

Askari wa zamani wa Marekani Vincent Emmanuele

Vincent Emanuele, askari wa zamani wa Kimarekani aliyehudumu katika vita vya Iraq kuanzia mwaka 2003 hadi 2011 ameeleza katika barua yake hiyo kwamba: Nikiwa mwanajeshi, nimesaidia katika kuanzishwa kwa Daesh na katika jinai zilizofanywa na jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati na kupelekea kuibuka kwa Daesh. 

Kuungama huko kwa veterani huyo wa Marekani katika vita vya Iraq, ni mfano mmoja tu wa undumakuwili wa Marekani katika kupambana na ugaidi, huku kukiwepo na mifano kadhaa inayothibitisha kuwa Marekani si mkweli katika suala la kupambana na baa hilo. Kuhusiana na nukta hiyo, Ahmad Musavi Muballegh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema: Marekani haijaonyesha kuwa ni mkweli katika kupambana na ugaidi ikiwemo nchini Afghanistan. 

Mfano mwingine unaodhihirisha uzandiki na unafiki wa Marekani katika kupambana na ugaidi ni uungaji mkono wake kwa Saudi Arabia, ambayo ni kitovu cha uenezaji ugaidi duniani. Japokuwa utawala wa Aal Saud umekuwa na nafasi hasi na haribifu katika eneo la Magharibi ya Asia kutokana na kuwafadhili na kuwaunga mkono magaidi, lakini unaungwa mkono kikamilifu na Marekani, ambapo hata katika vita vamizi ilivyoanzisha dhidi ya Yemen pia imepata baraka na uungaji mkono kamili wa Washington.

Kutokana na yote hayo tunaweza kusema kuwa, undumilakuwili wa Marekani katika kupambana na ugaidi na uungaji mkono wake kwa siasa haribifu za utawala wa Saudia katika eneo la Magharibi ya Asia pamoja na vita dhidi ya Yemen, na wakati huo huo kuzusha tuhuma hewa dhidi ya Iran, ni ishara ya ukubwa wa uhasama, chuki na uadui walionao viongozi wa Marekani kwa wananchi na serikali ya Iran, kwa sababu ya msimamo taifa hili wa kujichukulia maamuzi kwa kujitegemea na bila kujali matakwa ya utawala wa Washington.../