Iran yatahadharisha: Israel inaunda muungano na magaidi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetahadharisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel, ambao unatoa uungaji mkono kwa magaidi nchini Syria, unaweza kuunda muungano na magaidi hao iwapo tishio lao halitashughulikiwa ipasavyo.
Tahadhari hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Iran katika Umoja wa Mataifa Es’haq Al-e Habib wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao kuhusu 'tishio kwa amani na usalama wa kimataifa litokanalo na vitendo vya kigaidi na kukabiliana na ufadhili wa kifedha wa ugaidi."
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema, iwapo hatua hazitachukuliwa, basi kuna uwezekano kuwa magaidi na maghasibu (Israel) watageuka na kuwa muungano. Amesema tayari hatua za awali za muungano huo zimeshachukuliwa, kwani Israel inawaunga mkono magaidi nchini Syria kwa njia mbali mbali kama kuwapa huduma za tiba magaidi hao ambao inawatazama kama ndugu.
Magazeti ya Uingereza yamewahi kufichua kuwa magaidi wakufurishaji waliojeruhiwa vitani Syria hupata matibabu katika hospitali za Israel na hilo limekuwa likifanyika tokea vita hivyo vianze mwaka 2011. Aidha katika mahojiano na gazeti la The Sunday Times, mkuu wa zamani wa majeshi ya Israel Luteni Jenerali Gadi Eizenkot alikiri kuwa utawala wa Israel umekuwa ukiwapa silaha 'nyepesi' magaidi nchini Syria.
Katika kikao hicho cha Alhamisi , Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la aina yake ambalo linazuia ufadhili wa makundi ya kigaidi kote ulimwenguni.