Iran yamshangaa Netanyahu kwa kutiwa kiwewe na safari ya Shinzo Abe nchini
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemkejeli na kumshangaa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa kuingiwa na kiwewe kutokana na safari tarajiwa ya Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Japan hapa mjini Tehran.
Alaeddin Borujerdi ameashiria mazungumzo ya simu ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe kabla ya kuanza safari yake hapa Tehran na kubainisha kuwa, haelewi ni kwa nini Netanyahu anapinga safari hiyo ya kidiplomasia ya Waziri Mkuu wa Japan hapa nchini yenye lengo la kupunguza msuguano kati ya Iran na Marekani.
Boroujerdi amefafanua kwa kusema, "China, Russia na India zimeendelea kuwa na uhusiano mzuri na Iran licha ya mashinikizo ya Marekani, na hivi sasa utawala wa Kizayuni unahofia kuwa yumkini Japan ikajiunga na timu hiyo."
Amesema Waziri Mkuu wa Japan anakuja nchini kuzungumzia msuguano huo wa Marekani na Iran na vile vile makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini haji nchini kama mpatanishi wa Tehran na Washington.
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, mashinikizo yote ya Marekani dhidi ya Iran yanakusudia kuilazimisha Tehran ibadili sera zake za kieneo na isiimarishe mfumo wake wa makombora ya ulinzi, lakini Washington inatumia kisingizio cha 'mabomu ya nyuklia'.
Ameongeza kuwa safari ya Abe hapa nchini itazungumzia pia masuala ya kieneo na kimataifa, pamoja na uhusiano wa pande mbili wa Tokyo na Tehran.