Rais Rouhani: Nchi za Ulaya zina muda mfupi wa kuiokoa JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54183-rais_rouhani_nchi_za_ulaya_zina_muda_mfupi_wa_kuiokoa_jcpoa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Ulaya zina muda mfupi wa kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2019 08:34 UTC
  • Rais Rouhani: Nchi za Ulaya zina muda mfupi wa kuiokoa JCPOA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Ulaya zina muda mfupi wa kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumatatu wakati akimpokea balozi mpya wa Ufaransa hapa Tehran,  Philippe Thiébaud, ambapo amezitaka nchi za Umoja wa Ulaya zitekeleze wajibu wao katika makubaliano hayo.

Amebainisha kuwa, "Huu ni wakati nyeti, Ufaransa na nchi nyingine zilizosalia kwenye JCPOA zinaweza kutekeleza wajibu wa kihistoria wa kuyaokoa mapatano hayo katika kipindi hiki kifupi kilichosalia."

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, kuvunjika kwa makubalino hayo hakutakuwa kwa maslahi ya yeyote, kieneo na kimataifa.

Terehe 8 mwezi uliopita wakati ambapo Marekani ilikuwa inaadhimisha mwaka mmoja tangu ijiondoe kwenye makubaliano ya JCPOA, Rais wa Iran alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu imesimamisha kwa muda wa siku 60 uuzaji nje wa urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito, ikiwa ni katika kupunguza ushirikiano wake kwenye mapatano hayo.

Dakta Rouhani alisema Iran imeziambia nchi wanachama wa mapatano hayo ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia na China kuwa zina muhula wa siku 60 wa kutekeleza wajibu wao katika makubaliano hayo, vinginevyo Iran itachukua hatua zaidi.

Rais Rouhani na balozi mpya wa Ufaransa mjini Tehran

Kwengineko katika mazungumzo yake na balozi mpya wa Ufaransa hapa Tehran,  Rais Rouhani amesema hakuna kizingiti chochote kinachokwamisha uimarishwaji wa uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Paris, hususan katika uga wa uchumi.

Kwa upande wake balozi wa Ufaransa mjini Tehran Philippe Thiébaud amesema nchi hiyo iko tayari kuboresha uhusiano wenye maslahi ya pande mbili wa Ufarasa na Iran, na kusisitiza kuwa nchi hiyo ya Ulaya inafanya kila linalowezekana kuinusuru JCPOA.