Iran inashirikiana kiuchumi na zaidi ya nchi 70 duniani
(last modified Sat, 22 Jun 2019 07:22:27 GMT )
Jun 22, 2019 07:22 UTC
  • Iran inashirikiana kiuchumi na zaidi ya nchi 70 duniani

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na zaidi ya nchi 70 duniani.

Hayo yamedokezwa siku ya Ijumaa na Gholamreza Ansari Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia udiplomasia wa kiuchumi wakati akizungumza pembizoni mwa kikao cha ushirikiano wa Iran na Uturuki mjini Isfahan. Ansari ameongeza kuwa, kuundwa tume za pamoja za ushirikiano wa kiuchumi na nchi hizo ni sababu muhimu ya kuimarika uchumi wa Iran. 

Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, ushirikiano wa karibu na nchi jirani ni jambo lenye umuhimu mkubwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia udiplomasia wa kiuchumi ameongeza kuwa, hivi sasa asilimia 95 ya mabadilishano ya kimataifa ya kibiashara katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanahusu nchi jirani na yaliyosalia yanajumuisha nchi kama vile China na India.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (kushoto) na mwenzake wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu

Hali kadhalika amesema balozi na ofisi za kidiplomasia za Iran nje ya nchi zina uwezo wa kuwaunganisha wafanyabiashara Wairani na vituo vya kimataifa vya kibiashara.

Mkutano wa ushirikiano kati ya Iran na Uturuki ulifanyika Ijumaa mjini Isfahan na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na mwenzake wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu. Katika kikao hicho, nchi mbili zilitiliana saini mapatano kadhaa ya ushirikiano.