Iran: Vikwazo vipya vinaashiria namna Marekani isivyoheshimu sheria za kimataifa
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ni ithibati nyingine tosha kuwa utawala wa Washington hauko tayari kuheshimu sheria za kimataifa.
Majid Takht-Ravanchi aliyasema hayo jana Jumatatu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kusisitiza kuwa, Marekani inapaswa kusitisha vita vyake vya kiuchumi na ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran.
Amemshangaa Rais Donald Trump ambaye anasema Marekani iko tayari kufanya mazungumzo na Iran katika hali ambayo utawala wake umeshadidisha vikwazo na mashinikizo dhidi ya taifa hili.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kwamba, kamwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kuburuzwa kwenye meza ya mazungumzo kwa kutumia mashinikizo na ugaidi wa kiuchumi.
Mwandiplomasia huyo wa Iran amekumbusha kuwa, kujiondoa Marekani katika mpatano ya nyuklia ya JCPOA ulikuwa ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa hasa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivi sasa Washington inafuatilia kukanyaga sheria na maazimio yote ya kimataifa.
Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeukosoa vikali utawala wa Trump kwa kuendelea kukiuka jitihada za jamii ya kimataifa za kunusuru amani na usalama wa dunia.
Msemaji wa wizara hiyo, Abbas Mousavi ameashiria Mkataba wa Umoja wa Mataifa uliopasishwa na viongozi wa dunia mwaka 1942 unaotaka kuheshimiwa viongozi wa nchi huru na kufafanua, "Vikwazo vya kipuuzi dhidi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Ayatullah Ali Khamenei) na kamanda wa diplomasia wa Iran (Mohammad Javad Zarif) vina maana ya kufungwa kabisa mlango wa udiplomasia na utawala uliochanganyikiwa wa Washington."
Waziri wa Hazina ya Taifa wa Marekani, Steven Mnuchin amefafanua vikwazo vipya viliyosainiwa na Trump jana Jumatatu na kusema, vitailenga moja kwa moja Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Ali-Reza Tangsiri, kamanda mkuu wa Kikosi cha Majini cha Jeshi wa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kamanda mkuu wa Kikosi cha Anga cha SEPAH, Brigedia Jenwerali Amir-Ali Hajizadeh na Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour na kamanda mkuu wa Kikosi cha Nchi Kavu cha jeshi hilo la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mnuchin amesema Dakta Zarif atakabiliwa na vikwazo hivyo vya Marekani baadaye wiki hii.