'Kutunguliwa droni ya Marekani kumeibua fahari, izza na ghera ya Wairani'
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kutunguliwa ndege isiyo na rubani (drone) ya Marekani baada ya kukiuka anga ya Iran ni jambo ambalo limeibua ghera, izza na furaha ya Wairani.
Akizungumza Jumanne ya leo, Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaonyesha huruma wala mchezo hata kidogo katika kulinda maslahi yake ya kitaifa.
Ameendelea kusema kuwa, maadui wa Iran ya Kiislamu leo wanafahamu kikamilifu kuhusu uwezo wa kiulinzi wa mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo hawana uwezo wa kutekeleza chokochoko za kijeshi.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza alfajiri ya siku ya Alkhamisi iliyopita kwamba, kikosi cha anga cha jeshi hilo kiliitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani baada ya kukiuka sheria na kuingia katika anga ya Iran kwenye mkoa wa Hormuzgan katika Ghuba ya Uajemi.
Jeshi la Iran lilitungua ndege isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk ambayo ni miongoni mwa ndege za kisasa kabisa za ujasusi za Marekani na inayogharimu dola milioni 220. Kutumwa kwa ndege hiyo ya kijasusi katika anga ya Iran ni hatua ya kichochezi inayoonyesha kuwa, Marekani ndiyo mchafuzi na mvurugaji mkuu wa amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Iran imezitoa za mfumo wa kimataifa wa GPS, drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilikuwa katika anga ya Iran wakati wa kutunguliwa. Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti droni hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa.