Kamanda wa IRGC: Marekani haina ubavu na ujasiri wa kuishambulia Iran
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema hakuna nchi yoyote ile duniani ikiwemo Marekani yenye ujasiri, ubavu na uthubutu wa kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Anga cha SEPAH amewataka Wamarekani wachunge mienendo yao ghalati, akisisitiza kuwa sio kila nchi iko tayari kufuata amri, maagizo na matakwa ya Washington kila mara.
Brigedia Jenerali Hajizadeh amesema Marekani imekuwa ikipuuza uwezo mkubwa wa kujilinda Iran, na ndiposa walichanganyikiwa kutokana na jibu la hivi karibuni la Iran ilipokiuka anga ya nchi hii.
Siku chache zilizopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitungua ndege isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk ambayo ni miongoni mwa ndege za kisasa kabisa za ujasusi za Marekani na inayogharimu dola milioni 220, baada ya kukiuka sheria na kuingia katika anga ya Iran.
Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti droni hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa.
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, "Hawakutarajia kabisa jibu kali tulilowapa, baada ya kuvunja sheria za kimataifa na kukiuka anga yetu. Tulitoa onyo kadhaa kabla ya kuitungua droni yao ya RQ-4 Global Hawk mnamo Juni 20."