Zarif amjibu Trump, asema 'vita vifupi na Iran' ni njozi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja kama njozi na ndoto za alinacha matamshi ya Rais Donald Trump ambaye amedai kuwa iwapo Marekani itaingia katika vita na Iran, basi vita hivyo havitadumu kwa muda mrefu.
Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Vita vifupi na Iran ni njozi, yule atakayeanzisha vita, sio yeye atakayevimaliza."
Katika ujumbe wake huo, Dakta Zarif ameashiria kuhusu sera za vikwazo za utawala wa Trump dhidi ya taifa la Iran na kubainisha kuwa, vikwazo sio mbadala wa vita, bali ni vita halisi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemshangaa Trump ambaye kwa upande mmoja anadai kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Tehran na kwa upande mwingine anaendelea kulishinikiza taifa hili. Amesema vitisho na mazungumzo ni vitu visivyotangamana.
Kadhalika Mohammad Javad Zarif amekosoa vikali kauli ya Trump aliyedai kuwa, iwapo Marekani itaingia vitani na Iran, basi itaifuta kikamilifu nchi hii. Amesema "Matamshi hayo ni sawa na mauaji ya kimbari ambayo ni jinai ya kivita."
Hapo jana Jumatano katika mahojiano na televisheni ya CNN, Dakta Zarif alipuuzilia mbali kauli hiyo ya Trump ya kuifuta Iran katika uso wa dunia, na kusisitiza kuwa hilo linawezekana tu iwapo Marekani itatumia silaha haramu zilizopigwa marufuku.