Russia yaunga mkono mazungumzo baina ya Iran na nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54540-russia_yaunga_mkono_mazungumzo_baina_ya_iran_na_nchi_za_kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, anaunga mkono na kushajiisha mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2019 02:58 UTC
  • Russia yaunga mkono mazungumzo baina ya Iran na nchi za Kiarabu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, anaunga mkono na kushajiisha mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Kiarabu.

Sergey Lavrov amesema kuwa, kuna udhaura wa kuwepo mazungumzo baina ya Iran na nchi za Kiarabu katika suala la usalama na amani ya eneo la Mashariki ya Kati.

Lavrov ameongeza kuwa, mazungumzo hayo yanapaswa kufanyika kwa shabaha ya kujenga hali ya kuaminiana baina ya Iran na nchi za Kiarabu na kuleta uwazi katika masuala yanayohusiana na usalama na amani.

Baadhi ya nchi za Kiarabu za magharibi mwa Asia zimekuwa zikifuata kibubusa sera na siasa za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusababisha mivutano isiyo na msingi katika kanda ya Mashariki ya Kati. 

Muhammad Javad Zarif

Siku chache zilizopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif aliandika makala katika gazeti la Kuwait la al Rai na kutoa pendekezo la kuanzishwa Jukwaa la Mazungumzo ya Kikanda katika eneo la magharibi mwa Asia kwa ajili ya kusaidia jitihada za kutafuta utatuzi wa matatizo ya eneo hilo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na maradhi mawili ya saratani yaani ugaidi na misimami ya kufurutu mipaka.