Iran na Uganda kuimarisha uhusiano wao wa kiutamaduni
Waziri wa Jinsia na Utamaduni wa Uganda amesema nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina hamu ya kuimarisha uhusiano wake wa kiutamaduni na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Peace Mutuuzo amesema hayo mjini Kampala katika mazungumzo yake na Mohammadreza Ghezelselfi, Afisa Mkuu wa Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda na kuongeza kuwa, Kampala inataka kustafidi na utajiri mkubwa wa tajriba ya utamaduni wa Iran.
Amesema, "Serikali na taifa la Uganda linaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina utamaduni wa kihistoria, hivyo pande mbili zinaweza kuimarisha ushirikiano wao katika uga huo."
Waziri wa Jinsia na Utamaduni wa Uganda ametoa pendekezo la kuundwa 'chumba cha utamaduni' katika Kamisheni ya Pamoja ya Utamaduni ya Iran na Uganda. Hali kadhalika ameashiria juu ya uwezekano wa Uganda kuanza kufunza lugha ya Kifarsi katika vyuo na taasisi zake za elimu.
Maafisa wa serikali ya Kampala wamekuwa wakisisitiza juu ya ulazima wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa Iran na Uganda katika nyuga tofauti.
Katika mkutano wa mwishoni mwa mwezi Februri mwaka huu mjini Kampala, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda na Seyed Morteza Mortazavi, Balozi wa Iran mjini Kampala walibainisha kuwa, nchi mbili hizi zitaendelea kuimarisha uhusiano wa pande mbili hususan katika nyuga za uchumi, utalii na biashara.