Iran: Hakuna mazungumzo yoyote baina yetu na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haifanyi mazungumzo ya kiwango chochote kile na viongozi wa Marekani.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu madai kwamba, Marekani imetuma ujumbe wa mazungumzo na Iran kupitia Russia katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili.
Siku chache zilizopita, baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa ikieneza taarifa kwamba kuna mazungumzo baina ya Iran na Marekani kwa upatanishi wa Russia.
Wakati huo huo ujumbe wa bunge la Marekani katika kikao cha Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki huko Vienna ulitoa tamko siku ya Jumatano ya tarehe 10 Julai ukidai kuwa, Washington iko tayari kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya masharti yoyote.
Katika upande mwingine, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amezungumzia kuendelea kutengwa Marekani kimataifa na kusema kuwa, ukitoa nchi moja au mbili, nchi zote wanachama wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) zilipuuza njama za Marekani dhidi ya Iran katika kikao chao cha hivi karibuni.
Rais Rouhani amesema hayo katika mji wa Shirvan, mkoani Khorasan Kaskazini huko kaskazini mashariki mwa Iran ambapo ameeleza bayana kuwa, licha ya Marekani kuitisha kikao maalumu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) hivi karibuni, lakini njama zake dhidi ya Iran kwa kutumia bodi hiyo zilifeli.