Zarif: Iran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54798-zarif_iran_haitofanya_tena_mazungumzo_kuhusu_mapatano_ya_nyuklia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2019 05:25 UTC
  • Zarif: Iran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia.

Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya BBC na kujibu swali kuhusu kwa nini hakufanyiki mazungumzo mengine ya nyuklia akisema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siyo iliyojitoa katika mazungumzo, bali ni Marekani ndiyo iliyojitoa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesisitiza kuwa, ni kweli rais wa Marekani, Donald Trump hataki vita, lakini kuna watu ndani ya serikali yake ni wendawazimu na wana kiu ya kuanzisha vita.

JCPOA

 

Aidha amesema kuwa, kama vita vitatokea, kwa hakika hakuna nchi yoyote katika eneo hili itakayobaki salama, hivyo kila mtu ana wajibu wa kuchukua hatua na kufanya juhudi za kujiepusha kabisa na vita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekwenda mjini New York, Marekani kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha viongozi wa ngazi za juu wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ambapo ajenda yake mwaka huu ni kujadili hati ya ustawi endelevu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwanachama wa baraza hilo tangu mwaka huu wa 2019 na Dk Mohammad Javad Zarif anatarajiwa kuhutubia kikao cha baraza hilo.