Araqchi: Labda Wamarekani wametungua droni yao wenyewe kwa kudhani ni ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54859-araqchi_labda_wamarekani_wametungua_droni_yao_wenyewe_kwa_kudhani_ni_ya_iran
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu madai ya rais wa Marekani ya kwamba meli ya kivita ya nchi hiyo eti imetungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, pengine Wamarekani wametungua droni yao wenyewe kwa kudhani ni ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2019 03:08 UTC
  • Araqchi: Labda Wamarekani wametungua droni yao wenyewe kwa kudhani ni ya Iran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu madai ya rais wa Marekani ya kwamba meli ya kivita ya nchi hiyo eti imetungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, pengine Wamarekani wametungua droni yao wenyewe kwa kudhani ni ya Iran.

Rais wa Marekani, Donald Trump jana Alkhamisi alidai kuwa, manuwari ya kivita ya USS Boxer imetungua ndege moja ndogo ya Iran isiyo na rubani ambayo ilikuwa imeikaribia manuwari hiyo. Madai hayo ya Trump yametolewa katika hali ambayo hata taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani yenyewe haikuashiria kabisa kuwa droni inayodaiwa kutunguliwa na manuwari hiyo ilikuwa ya Iran.

Akijibu madai hayo yasiyo na msingi ya Trump, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema leo katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, huenda manuwari ya kivita ya Marekani ya USS Boxer imetungua kimakosa droni ya Marekani yenyewe.

USS Boxer

 

Kabla ya hapo pia, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa amesema kwamba, hakuna taarifa zozote zinazoonesha kwamba Iran imepoteza ndege yake isiyo na rubani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Wakati huo huo msemaji mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha vikali madai hayo ya rais wa Marekani na kusema kuwa yanatokana na njozi na ndoto tu za Donald Trump. Brigedia Jenerali Aboul Fazl Shekarchi amesema, kinyume kabisa na ndoto hizo za rais wa Marekani, ndege zisizo na rubani za Iran zimefanya operesheni zake za utafiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz na kurejea vituoni salama zikiwa zimekusanya taarifa za kina na hakujaripotiwa operesheni yoyote ya kushambuliwa na manuwari ya kivita ya Marekani ya USS Boxer.