Rouhani: Iran iko tayari kunyoosha mkono wa urafiki kwa jirani zake
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kunyoosha mkono wa urafiki kwa jirani zake, sambamba na kusamehe makosa yaliyofanywa na baadhi ya nchi hizo.
Rais Rouhani amesema hayo leo Jumapili akihutubia gwaride la majeshi ya Iran hapa Tehran, kwa mnasaba wa kuanza maadhimisho ya 39 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu.
Ameeleza bayana kuwa, "Maadui wa Uislamu wana hamu kubwa ya kutumia fursa na mwanya uliosababishwa na migawanyiko miongoni mwetu katika eneo kwa maslahi yao."
Dakta Rouhani amezitaka nchi ajinabi kuondoka mara moja katika eneo hili la Asia Magharibi iwapo ni wakweli katika matamshi yao, kwamba wanataka kuona usalama na uthabiti unaimarika katika eneo, badala ya kuligeuza eneo hili kuwa soko la silaha zao.
Kadhalika Rais wa Iran amesema atawasilisha katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 'Mpango wa Amani wa Hormuz" ambalo ni pendekezo la Tehran linaloainisha mikakati na fremu ya ushirikiano baina ya nchi za eneo kwa shabaha ya kuimarisha usalama na uthabiti.
Amesema vikosi vya Marekani ndivyo vimeyumbisha usalama na amani katika nchi za Afghanistan, Syria, Iraq na Ghuba ya Uajemi.
Rais Hassan Rouhani anatazamiwa kuelekea New York kushiriki mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatatu.