Oct 24, 2019 12:15 UTC
  • Haki za Binadamu; mchezo mchafu wa siasa za Magharibi dhidi ya Iran

Moja ya silaha zinazotumiwa na Magharibi katika kuamiliana na nchi zenye misimamo huru ni kutumia maudhui ya haki za binadamu; na katika hilo, mtazamo wa upande mmoja tu na wa Kimagharibi kwa maudhui hiyo katika jamii ambayo ni ya Kiislamu, inayojitawala na yenye misimamo huru ni aina mojawapo ya undumakuwili unaombatana na siasa chafu.

Kuzitolea hukumu haki za binadamu kwa kutumia mtazamo wa aina moja tu wa Kimagharibi, bila kuzingatia chimbuko la utungaji sheria katika nchi inayokusudiwa na kuelewa ni usuli na misingi gani ya haki na sheria inayotumika katika nchi hiyo, ni jambo linalozifanya ripoti za haki za binadamu za upande mmoja zinazotolewa na taasisi za Magharibi zisiwe na thamani wala itibari yoyote.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, hivi karibuni alitoa agizo la utekelezaji wa siasa na sera kuu za mfumo wa utungaji sheria kwa wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola, ambapo alisistiza kwamba: Chimbuko la asili la utungaji sheria, katika kupanga na kupitisha kanuni na miswada ya sheria, ni kuzingatia vipimo vya sharia za dini.

Suratul-Fatihah

Katika suala la utungaji sheria, Iran, ambayo ni nchi ya Kiislamu, inaziangalia kwa jicho maalumu sharia za Uislamu ambazo zimebainishwa kwa uwazi ndani ya Kitabu cha mbinguni cha Waislamu cha Qur'ani Tukufu.

Misingi ya sharia za Uislamu inahisabiwa kuwa chimbuko kuu la utungaji sheria na kanuni nchini Iran; na ndiyo inayozingatiwa na vyombo vya mahakama na watungaji sheria katika masuala yote.

Muelekeo wa Kiislamu kwa suala la haki za binadamu, japokuwa katika baadhi ya masuala unatilia mkazo kutekelezwa bila mzaha hukumu ya sheria ya kifo na kisasi baada ya kupitia ngazi zote za kimahakama na tab'an kwa kufuata vipimo vya sharia za dini, lakini kiujumla unazingatia msingi wa uraufu na huruma ya Kiislamu.

"Aliye muuwa mtu... basi ni kama amewauwa watu wote."  

Kwa mfano, juhudi anazofanya hakimu kuinasihi familia inayotaka itekelezewe haki yake ya kisasi ikubali kusamehe haki yake hiyo, inadhihirisha kilele cha uraufu na huruma ya Kiislamu; na hili ni jambo linaloakisi tafsiri na maana tofauti ya haki za binadamu kulinganisha na vile zinavyoelezwa katika maandiko ya Magharibi.

Mtazamo wa sheria na kanuni unaofuata vipimo vya sharia za Uislamu unatafautiana na mtazamo wa sheria unaotawala katika Ulimwengu wa Magharibi; kwa hivyo haiwezekani kutumia muelekeo na tafsiri ya haki za binadamu ya Kimagharibi tu kwa ajili ya kuhakiki na kuzungumzia masuala ya haki na sheria katika nchi kama Iran.

Kuhusiana na nukta hii, Mohammad Hassaninejad, mwakilishi wa Iran katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema, ripoti mpya iliyotolewa na Javaid Rehman, ripota maalumu wa haki za binadamu wa umoja huo katika masuala ya Iran imeandaliwa ili kukidhi na kufuata sera ya ugaidi wa kiuchumi wa Marekani; na akasisitiza kwamba: Madikteta hawawezi kueleza chochote kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran. 

Mohammad Hassaninejad, mwakilishi wa Iran katika Kamati ya Tatu ya UNGA

Katika ripoti yake mpya aliyotoa jana Jumatano, Javaid Rehman, ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iran amekosoa tena utekelezwaji wa sheria ya Kiislamu ya kisasi na ya kifo kwa wafanyamagendo ya mihadarati, na kudai kwamba, haki za binadamu zinakiukwa hapa nchini.

Kama mtu yeyote yule atakuwa katika nafasi ya ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iran, ataizungumzia maudhui ya haki za binadamu nchini Iran kwa kutumia tafsiri ya Kimagharibi, wakati chimbuko na msingi mkuu wa utungaji sheria hapa nchini ni kufuata vipimo vya sharia za Uislamu.

Javaid Rehman

Kwa kumalizia, inapasa tuseme kuwa, madai ya kila siku yanayokaririwa na ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iran ni kielelezo cha siasa chafu na utumiaji mbaya wa suala la haki za binadamu unaofanywa na Magharibi katika kuamiliana na Iran.../ 

Tags