Zarif aikosoa US kwa kumwekea vikwazo ripota wa UN
Aliyekuwa Makamu wa Rais katika Masuala ya Kistratajia wa Iran, Mohammad-Javad Zarif amekosoa hatua ya Marekani ya kumuwekea vikwazo Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
"Katika uthibitisho zaidi wa hatua za kipuuzi za Marekani, Washington imemtoa kiongozi wa Al Qaeda nchini Syria kwenye orodha yake ya magaidi, na kumuwekea vikwazo Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu," Zarif ameandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X jana Alhamisi.
Dakta Zarif ambaye amewahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, hatua hiyo "si tofauti na mwaka 1984, wakati Marekani ilipomtoa Saddam (Hussein) na badala yake kuiweka Iran kwenye orodha yake ya ugaidi."
Zarif amehitimisha ujumbe wake huo kwenye mtandao wa X kwa heshtegi ya kutaka afisa huyo wa ngazi ya juu wa UN apewe tuzo ya amani yaNobe. Ameanikd: #NobelPeace4Albanese.
Juzi Jumatano, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio alitoa tamko la serikali kwa kusema: "Leo ninaweka vikwazo kwa Ripota Maalumu wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese kwa hatua zake zisizo halali na za kuaibisha kutaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ichukue hatua dhidi ya maafisa wa Marekani na Israel, makampuni na watendaji".
Akitoa radimali yake kwa tangazo hilo la Rubio, Katibu Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, Agnès Callamard amesema: "Hili ni shambulio lisilo na aibu na la wazi dhidi ya kanuni za msingi za haki za kimataifa. Maripota Maalum hawateuliwi ili kufurahisha serikali au kuwa maarufu bali kutekeleza majukumu yao."
Aliongeza, "Jukumu la Francesca Albanese ni kutetea haki za binadamu na sheria za kimataifa, muhimu zaidi wakati huu ambapo uhai wa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa kwa mabavu uko hatarini."
Amesema, "Vikwazo hivi vinakuja siku chache baada ya (Albanese) kuchapisha ripoti mpya inayoelezea jinsi makampuni yamefaidika kutokana na uvamizi haramu wa Israel, mfumo wake wa ubaguzi wa apartheid na mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza."