Trump aendeleza hatua za kiuadui katika sekta ya mafuta dhidi ya Iran
Rais Donald Trump wa Marekani ametaka zichukuliwe hatua kali zaidi za vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran ukiwa ni muendelezo wa hatua za kiuadui na uhasama za serikali ya Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kupitia taarifa aliyotoa mapema leo, Trump ameashiria hali ilivyo katika soko la mafuta na kusisitiza kutekelezwa hatua kali zaidi za vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran.
Katika taarifa yake hiyo, Rais wa Marekani ametoa agizo kwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo, waziri wa fedha Steven Mnuchin na waziri wa nishati Rick Perry la kuiwekea vikwazo vikali zaidi vya mafuta Iran kwa kutumia sheria ya mamlaka ya ulinzi wa taifa ya Marekani.
Agizo hilo la Trump limetolewa kwa lengo la kupunguza miamala ya mabadilishano ya mafuta kati ya Iran na taasisi za fedha za kigeni.
Licha ya hatua za kiuadui zinazochukuliwa na Trump na maafisa wa Ikulu ya White House dhidi ya Iran, nchi mbali mbali za Ulaya, China, Russia pamoja na wanunuzi wengine wa mafuta ya Iran wanaendelea kufanya mabadilishano ya kibiashara ya mafuta na Tehran.
Serikali ya Washington imetangaza kuwa, lengo la kuendesha kampeni ya "mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa" dhidi ya Iran ni kuweza kufikia mapatano mengine mapya na Tehran yatakayohusisha masuala yote inayotaka Marekani.
Hata hivyo serikali ya Iran imesisitiza kuwa, katika anga hiyo chafu ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa pamoja na kuendelea kuwekewa vikwazo vya nyuklia haitafanya mazungumzo hata katika kalibu ya kundi la 5+1.../