Rais Rouhani: Jopo la uchunguzi wa ajali ya ndege ya Ukraine libuniwe
(last modified Tue, 14 Jan 2020 12:04:37 GMT )
Jan 14, 2020 12:04 UTC
  • Rais Rouhani: Jopo la uchunguzi wa ajali ya ndege ya Ukraine libuniwe

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kuundwa jopo maalumu la mahakama la kuchunguza ajali ya ndege ya Ukraine iliyoua watu 176 siku chache zilizopita hapa jijini Tehran, sanjari na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa ajali hiyo.

Rais Rouhani amesema hayo leo pambizoni mwa Maonyesho ya Kilimo cha Ndani hapa Tehran ambapo amebainisha kuwa, "Idara ya Mahakama inapaswa kuunda jopo maalumu litakaloongozwa na jaji mwandamizi na makumi ya wataalamu, kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo."

Dakta Rouhani amesema, hii sio kesi ya kawaida na macho yote ya dunia yameelekezwa hapa nchini ili kufuatilia mchakato wa uchunguzi wa ajali hiyo. Kadhalika amezihakikishia familia za wahanga wa ajali hiyo kwamba serikali yake itafuatilia kadhia hii kwa uwezo na nguvu zake zote.

Rais Rouhani ameongeza kuwa, "ni hatua nzuri kwa vikosi vya usalama kukiri kosa lililotokea na kuomba radhi, lakini kile ambacho kila mmoja anataka kufahamu ni kuwa, je kosa hili lilifanyika katika mazingira yapi? Bila shaka kosa hili sio la mtu mmoja, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa kosa hilo la kibinadamu halikaririwi tena."

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Canada amesema wahanga 176 wa ajali hiyo wangelikuwa hai, iwapo kusingekuwa na taharuki katika eneo la Asia Magharibi.

Kipande cha mabaki ya ndege ya Ukraine iliyotunguliwa kimakosa Tehran

Justin Trudeau amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Global News na kuelekeza bayana kuwa, "nadhani kama kusingewepo na taharuki na kushadidi hali ya mambo katika eneo, raia hao wa Canada hii leo wangelikuwa nyumbani na familia zao."

Iran imeahidi kuzipa fidia familia za wahanga wa ajali hiyo ya ndege ya Ukraine sambamba na kushirikiana na pande kadhaa zinazochunguza mkasa huo wa kutunguliwa kimakosa ndege hiyo, wakati Iran ikilipiza kisasi cha kuuawa shahidi na Marekani, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).