Hatua ya kisiasa ya FATF ya kuiweka Iran katika orodha nyeusi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59316-hatua_ya_kisiasa_ya_fatf_ya_kuiweka_iran_katika_orodha_nyeusi
Nchi za Magharibi huku zikiongozwa na Marekani kwa muda sasa zimekuwa zikizingatia na kutilia maanani utekelezaji wa siasa za mashinikizo ya pande zote kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lengo likiwa ni kujaribu kubadilisha misingi na siasa za nchi hii.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 22, 2020 08:01 UTC
  • Hatua ya kisiasa ya FATF ya kuiweka Iran katika orodha nyeusi

Nchi za Magharibi huku zikiongozwa na Marekani kwa muda sasa zimekuwa zikizingatia na kutilia maanani utekelezaji wa siasa za mashinikizo ya pande zote kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lengo likiwa ni kujaribu kubadilisha misingi na siasa za nchi hii.

Kuhusiana na suala hilo kundi moja maalumu linalojiita kwa kifupi FATF ambalo linadai kupambana na utakatishaji wa fedha chafu kwa kimombo Financial Action Task Force (FATF)  jana Ijumaa Februari 21 lililiweka jina la Iran katika orodha yake nyeusi. Gazeti la Wall Street Journal awali liliripoti kuwa, uamuzi wa taasisi hiyo yenye makao yake Paris wa kujiunga na mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya Marekani dhidi ya Iran umepasishwa baada ya nchi ya Ulaya kuafiki jambo hilo.  Kundi hilo limetangaza wazi katika taarifa yake kwamba hatua hiyo dhidi ya Iran inaweza kubadilishwa, na nchi hii inaweza kuondolewa kwenye orodha nyeusi baada ya kupasishwa miswada husika. Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, kitendo cha kuiorodhesha Iran katika faharasa nyeusi ya FATF kimefanyika kwa namna ambayo milango bado iko wazi kwa Iran na haijafungwa kikamilifu. 

Kundi la FATF liliundwa mjini Paris Ufaransa mwaka 1989 kufuatia uamuzi wa wakuu wa kundi la G-7 na kwa madai eti ya kupambana na utakatishaji fedha. Wakuu wa G-7 walisema kuwa taasisi hiyo imeundwa lengo likiwa ni kuzifanya sawa sheria za kibenki na kupambana na vitendo vya utakatishaji fedha. Mwaka 2001 na baada ya matukio ya Septemba 11 huko Marekani taasisi ya FATF ilitoa kipaumbele zaidi kwa kile kilichotajwa kuwa ni mapambano dhidi ya njia za "kudhamini fedha za makundi ya kigaidi." Aidha kundi hilo limejipa jukumu la kusimamia utendaji wa kanali za kibenki katika ngazi ya kimataifa na ndani ya nchi za dunia likidai linapambana na utakatishaji wa fedha. 

Kundi la FATF liliasiwa mwaka 1989 mjini Paris, Ufaransa 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hata kama uamuzi huo wa FATF utaitia kwenye vizuizi gingi miamala ya kifedha ya Iran na kusababisha ukwamishaji mkubwa, lakini uamuzi huo hautakuwa na taathira ya maana kivitendo kwa sababu hivi sasa akthari ya benki za nchi Magharibi bila ya kujali makubaliano ya Iran na kundi la FATF; zimejizuia kufanya miamala ya kifedha na kibenki na Iran kwa kuzingatia vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran. Ni wazi kuwa, kundi la FATF limechukua hatua hiyo kwa chini ya mashinikizo ya Marekani kwa nchi za Ulaya.  

Viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya Trump kwa mara kadhaa walitaka Iran ijiunge na kundi hilo eti la kupambana na fedha chafu (FATF). Miongoni mwa viongozi hao ni Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ambaye Februari 12 mwaka huu aliitaka Iran ijiunge na Mkataba wa Kupambana na Ufadhili wa Fedha za Magaidi na Hati ya Palermo. Ikumbukwe kuwa kwa mtazamo wa Wamagharibi, kila kundi lisilokubali kuburuzwa na madola ya kibeberu hilo ni la kigaidi, lakini madola ya kibeberu yanayofanya mauaji dhidi ya raia na kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi za watu wengine, hizo si za kigaidi. Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana Pompeo alieleza kufurahishwa kwake baada ya kundi la FATF kuliweka jina la Iran katika orodha nyeusi. Huko nyuma pia maseneta wanne wa Marekani walidai katika barua waliyoituma kwa kundi hilo kwamba Iran haitofanya mabadiliko yoyote katika nyenendo zake licha ya kupita miaka miwili ya hatua ilizoainishiwa; na kwamba inapaswa kujumuishwa haraka iwezekanavyo kwenye faharasa nyeusi ya kundi eti la kupambana na utakatishaji wa fedha chafu la Financial Action Task Force (FATF).  

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Wakati huo huo Iran ilishasisitiza mara kadhaa kuwa Marekani na waitifaki wake wa kieneo wanafanya njama za kuiweka Iran katika orodha nyeusi ya kundi la FATF lengo likiwa ni kuibana Tehran. Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwahi kueleza kuwa: Serikali tatu zinaounga mkono ugaidi yaani Marekani, Saudi Arabia na Israel zimeazimia kuiweka Iran katika orodha nyeusi ya FATF.  Kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani cha kufurahia kuiwekwa Iran katika orodha nyeusi ya kundi hilo kinaonyesha kuwa Washington inalitumia kundi hilo kama wenzo wa kuzikandamiza zaidi kwa vikwazo nchi ambazo haziungi mkono siasa za Marekani ikiwemo Iran. 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Kinyume chake, Iran inaamini kuwa hatua ya kundi la FATF dhidi yake ni ya kisiasa kikamilifu na si ya kiadilifu. Sayyid Abbas Mousavi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, ni zaidi ya miaka miwili sasa ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza sheria na kanuni zote zinazohusiana na utakatishaji fedha na kudhamini fedha kwa ajili ya ugaidi na kuongeza kuwa Saudi Arabia ikiwa ndiyo benki kuu ya ugaidi na utawala wa Kizayuni ambayo ni serikali ya kigaidi, ndizo zinazofadhili pakubwa makundi na taasisi za kigaidi kote ulimwenguni.  Hata hivyo Iran ambayo inashirikiana zaidi katika masuala hayo na ambayo inaonesha uwazi wa kipekee, ndiyo inayojumuishwa katika orodha hiyo nyeusi ya FATF.