Iran yaboresha uwezo na kasi ya makombora yake ya baharini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60512-iran_yaboresha_uwezo_na_kasi_ya_makombora_yake_ya_baharini
Kamanda wa Kikosi cha Baharini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC amesema kikosi hicho kimeunda makombora yenye uwezo mkubwa zaidi, yanayoweza kupiga umbali wa kilomita 700.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Apr 21, 2020 08:11 UTC
  • Iran yaboresha uwezo na kasi ya makombora yake ya baharini

Kamanda wa Kikosi cha Baharini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC amesema kikosi hicho kimeunda makombora yenye uwezo mkubwa zaidi, yanayoweza kupiga umbali wa kilomita 700.

Admeri Alireza Tangsiri, Kamanda wa Kikosi cha Baharini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC amesema taifa hili limepata mafanikio hayo ya kuimarisha na kuboresha uwezo na kasi ya makombora yake bila kutegemea msaada wa nchi yoyote ile.

Amekumbusha kuwa, "kuna wakati makombora yetu ya baharini hayangepiga zaidi ya kilomita 45 licha ya (Iran) kusaidiwa na washauri wa kijeshi wa Marekani. Hata hivyo hivi sasa na kwa kutegemea wataalamu wetu wa kijeshi, tumefanikiwa kuunda makombora ya baharini hadi ardhini na ya ardhini hadi ardhini yenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 700."

Kamanda wa Kikosi cha Baharini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC amesema taifa hili linajivunia kupata mafanikio hayo yote katika uga wa kijeshi na kiulinzi kwa kuwategemea wataalamu na wasomi wa hapa nchini.

Sehemu ya makombora ya Iran

Haya yanajiri siku chache baada ya Admeri Hossein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusema kikosi hicho kinajiandaa kuunda nyambizi zitakazotumia nishati ya nyuklia zenye uwezo wa kutekeleza operesheni za baharini kwa muda mrefu zaidi katika maji ya kimataifa.

Aliashiria kuhusu mafanikio ya kikosi hicho katika uundaji anuai za vyombo na zana za majini na kueleza kwamba lengo ni kudhamini usalama na kuhakikisha kunakuwepo ulinzi kamili katika maeneo ya pwani ya Iran.