Iran yasema madai ya Marekani dhidi yake ni 'mzaha mchungu'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60807-iran_yasema_madai_ya_marekani_dhidi_yake_ni_'mzaha_mchungu'
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria juu ya uhusiano madhubuti baina ya taifa hili na Afghanistan, imekosoa vikali madai ya Marekani dhidi ya Tehran kuhusu tukio la kupoteza maisha raia wa Kiafghani katika eneo la Herat, mpakani mwa nchi mbili hizi.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 06, 2020 03:28 UTC
  • Iran yasema madai ya Marekani dhidi yake ni 'mzaha mchungu'

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria juu ya uhusiano madhubuti baina ya taifa hili na Afghanistan, imekosoa vikali madai ya Marekani dhidi ya Tehran kuhusu tukio la kupoteza maisha raia wa Kiafghani katika eneo la Herat, mpakani mwa nchi mbili hizi.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kitendo cha Marekani cha kuihusisha Iran na tukio hilo la Herat, mpakani mwa Iran na Afghanistan ni 'mzaha mchungu'.

Huku ikiashiria kuguswa na tukio hilo chungu la kuhuzunisha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeitaja Marekani kama utawala mtenda jinai nchini Afghanistan na muungaji mkono wa ugaidi kote duniani.

Mapema jana Jumanne, ubalozi wa Marekani mjini Kabul ulijidai kuonyesha wasi wasi wake juu ya tukio hllo la Herat na eti kudhulumiwa wahamiaji wa Kiafghani katika mpaka wa Iran. Hii ni katika hali ambayo, askari vamizi wa Marekani kwa miaka kadhaa sasa wanaendelea kufanya mauaji, ukandamizaji, ubakaji na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Kadhalika ubalozi huo wa US nchini Afghanistan ulidai kuwa unaunga mkono hatua ya serikali ya Kabul ya kuanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo.

Iran ni mwenyeji wa mamilioni ya raia wa Afghanistan

Hii ni katika hali ambayo, Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema tukio hilo la kupoteza maisha Waafghani lilifanyika katika ardhi ya Afghanistan, na Gadi ya Mpakani ya Iran imekanusha madai kuwa lilifanyika katika ardhi ya nchi hii.

Baadhi ya vyombo vya habari vimeeneza habari za propaganda zinazodai kuwa, raia kadhaa wa Afghanistan waliojaribu kuingia Iran kinyume cha sheria walikamatwa na askari wa mpakani wa nchi hii na kisha kuzamishwa kwenye Mto Hari katika eneo la Herat, mpakani mwa nchi mbili hizi; madai ambayo serikali ya Tehran imeyapuuzilia mbali.