Utawala wa Marekani unaongoza ugaidi wa kitiba dhidi ya Iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeikosoa vikali Marekani kwa kuongoza kampeni ya kimataifa ya kutekeleza ugaidi wa kiuchumi na kitiba dhidi ya haki za binadamu za taifa la Iran.
Katika taarifa kupitia Twitter Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje imeashiria ukiuwaji mkubwa wa haki za binadamu unaotekelezwa na utawala wa Marekani.
Taarifa hiyo imesema utawala wa Marekani unainyima Iran haki ya kuchukua fedha zake zilizo katika benki za kimataifa ili kukidhi mahitaji yake. Aidha Marekani pia imezuia vifaa vya kitiba vya COVID-19 ambavyo ni muhimu katika kuokoa maisha ya Wairani na hivyo ni wazi kuwa utawala wa Marekani unaongoza kampeni ya kimataifa ya ugaidi wa kiuchumi, na kitiba ambao unalenga haki za binadamu za taifa la Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kila mwaka kuanzia Juni 26 hadi Julai 2 Wairani hukumbuka ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaotekelezwa na Marekani.
Iran ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19 baada ugonjwa huo kuibuka China Disemba 2019. Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani vimezuia Iran kukabiliana vilivyo na ugonjwa wa COVID-19.
Mapema mwezi huu Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki alipongeza jitihada za Iran za kukabiliana na janga la COVID-19 na kuongeza kuwa Iran sasa inabadilisha vikwazo kuwa furasa na sasa inajitegenezea vifaa vingi vya kitiba na hata inaviuza nje ya nchi pamoja na kuwepo vikwazo hivyo haramu vya Marekani.