Iran kuzalisha makombora ya masafa marefu karibuni
Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kikosi hicho kitazalisha makombora ya masafa marefu hivi karibuni.
Brigedia Jenerali Yousef Ghorbani amesema hivi karibuni Iran itatangaza mafanikio makubwa katika uga wa kiulinzi, kwa kuzalisha makombora ya masafa marefu ya kilomita 20 na kilomita 200.
Amesema Jeshi la Anga la Iran limepiga hatua kubwa tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, na litaendelea kulilinda taifa hili kwa nguvu zake zote.
Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya taifa hili vimeendelea kupiga hatua na kupata mafanikio makubwa licha ya mashinikizo ya maadui.
Mwezi uliopita, Jeshi la Baharini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyia majaribio kwa mafanikio makombora yake mapya ya cruise ya masafa mafupi na yale ya masafa marefu katika luteka ya kijeshi iliyofanyika kaskazini mwa Bahari ya Hindi na katika Bahari ya Oman.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa, uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.